TANI 160 ZA KUNI NA MKAA ZINATUMIKA KILA SIKU KWENYE KAMBI ZA WAKIMBIZI KIGOMA..KANALI NDAGALA AFUNGUKA


Imeelezwa kuwa zaidi ya tani 160 za matumizi ya nishati ya kuni na mkaa hutumika katika kambi za wakimbizi mkoani Kigoma kwa siku moja, kwa matumizi ya kupikia hali inayo sababisha uharibifu wa mazingira katika maeneo yaliyo karibu na kambi hizo.

Hayo yalibainika leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani , yaliyofanyika mkoani Kigoma katika Kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu.

Mratibu wa Mradi wa utunzaji wa Mazingira Kambini CEMDO Tanzania Frank Kayegameni akitoa taarifa ya mradi huo alisema kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi kambi ya Nyarugusu ambayo imesababisha uhitaji mkubwa wa matumizi ya mazao ya misitu na kupelekea wakimbizi kutoka kwenda kutafuta kuni nje ya kambi kukata miti ambapo kwa siku inakadiriwa mtu mmoja anatumia kiasi cha kuni kilo moja ambapo kambi inakadiriwa kuwa na wakimbizi 152,309 hivyo kupelekea uharibifu mkubwa.

Alisema katika kupambana na hali hiyo shirika la uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa mazingira kambini ( CEMDO) Tanzania, kwa kushirikiana na Shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR wameandaa utaratibu wa upandaji wa miti 1,425,223 katika vijiji 13 vinavyozunguka Kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu kwa mwaka 2017/2018 , kugawa majiko banifu kwa kaya 9,600 za wakimbizi.

Mambo mengine ni majaribio ya ugawaji wa gesi kwa kaya 3180 lengo likiwa ni kupunguza matumizi ya nishati ya mkaa na kuni yanayopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kuboresha mazingira kutokana na uharibifu mkubwa wa uoto wa asili unaotokana na ukataji miti ovyo.

Akizungumza kwa  niaba ya mkuu wa mkoa wa Kigoma, Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya mazingira ni "Mkaa ni gharama; tumia nishati mbadala" inasaidia utunzaji wa misitu na mazingira, lakini kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakimbizi kupewa majiko banifu na gesi kwenda kuuza kwa Watanzania ili kujipatia fedha na kuendelea kuharibu mazingira na kuwataka wakimbizi kuacha tabia hiyo na kuendelea kutumia majiko yaliyotolewa na shirika hilo.

Kanali Ndagala alisema amefurahishwa na shughuli zilizotajwa na mashirika hayo ya kutunza mazingira na kuwaomba kuongeza utaalamu wa kutumia misitu kwa ufugaji wa nyuki, kwani ufugaji wa nyuki utawaletea kipato na kuongeza uchumi wao kwa ngazi ya kaya na mtu mmoja.

Aidha aliwashukuru kwa kazi kubwa ya kuelimisha jamii kutambua umuhimu wa kutunza mazingira kwa mkoa huo jamii imekuwa na tabia ya uharibifu wa mazingira hasa kwa kuchoma moto misitu.

"Lakini pia kupitia maadhimisho haya nitoe rai kwa wataalamu na viongozi mbalimbali katika halmashauri kusimamia kwa makini kilimo na shughuli za maendeleo, ili jamii ambazo zimekuwa chanzo cha uharibifu wa vyanzo vya maji ziweze kuhifadhi vyanzo vya maji, hili halina mjadala sheria zipo wazi wachukuliwe sheria wale wote wanaolima au kufanya shughuli za kijamii hatarishi katika vyanzo vya maji",

 "Suala la uchomaji moto misitu suala hili wahusika wote pamoja na viongozi walio katika eneo lililochomwa watachukuliwa hatua, lazima tutunze mazingira kwa maendeleo ya Nchi yetu hili ni agizo", alisema kanali Ndagala.

Naye Rais wa Wakimbizi kambi ya Nyarugusu Abilola Angelique alisema wao kama wakimbizi hawana budi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na mashirika yanayo wahudumia, kwa kuwa wanapotunza mazingira hata wao wanaendelea kunufaika kwa kuwa watatumia ardhi hiyo kulima mazao ya mboga mboga kwa ajili ya kujikimu na watoto wao, na kuwaomba wakimbizi wenzake kuendelea kusimamia utunzaji wa mazingira.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akihutubia wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira duniani leo. Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea  Ndagala akipokea maelezo ya mazao ya mboga mboga yanayolimwa na wakimbizi Kambi ya Nyarugusu katika mradi wa utunzaji wa mazingira

Mkuu wa wilaya ya Kakonko kanali Ndagala akioneshwa na Afisa wa Shirika la CEMDO majiko banifu yanayotumia kuni chache kwa lengo la kutokomeza uharibifu wa mazingira.
Mkimbizi akimuelezea mkuu wa wilaya namna wanavyo yatumia majiko banifu kuhakikisha hawaharibu mazingira

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527