MMOJA AFARIKI BASI LIKINUSURIKA KUTUMBUKIA ZIWA VICTORIA

Mtu mmoja amefariki na wengine zaidi ya 30 wakiponea chupuchupu kuzama Ziwa Victoria, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kufeli breki.

Hata hivyo, dereva wa basi hilo la Kampuni ya Sabco alifanikiwa kulielekeza basi hilo kwenye ukuta wa ofisi za Kivuko cha Kigongo-Busisi, wilayani Misungwi.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Mkadam Mkadam amesema ajali hiyo imetokea saa saba na robo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine 31 kujeruhiwa kati yao 10 walihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando. 

Dereva wa basi hilo, Idd Omary alijeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali ya misheni Bukumbi kwa ajili ya matibabu.

Kamanda Mkadam ametaja chanzo cha ajali hiyo ni basi hilo kufeli breki na hivyo dereva akalazimika kulibamiza kwenye ukuta wa ofisi ya Temesa. 

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Misheni Bukumbi, Deusdedith Baluhya amesema amepokea majeruhi 32 na mmoja amefariki dunia. 

Amesema kati ya majeruhi hao, wapo watoto wanne wenye umri wa chini ya miaka mitano, kati yao wakike ni watatu na wakiume mmoja.

Na Ngollo John na Johari Shani, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527