MKUTANO WA RAIS WA ZIMBABWE WAPIGWA BOMU

Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amenusurika kifo wakati kitu kinachohisiwa kuwa ni bomu kulipuka baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa White City, Bulawayo.


Video zilizotumwa mitandaoni zinawaonyesha wahudumu wa afya wakikimbilia eneo la tukio.


Msemaji wake, George Charamba ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa Rais huyo yupo salama na tayari amepelekwa katika Ikulu ya Bulawayo.


“Imetokea ajali katika eneo la Bulawayo, (White City Stadium) ambako Rais alikuwa akihutubia. Hili ni suala la polisi zaidi ingawa Rais yupo salama,” amesema Charamba huku akibainisha kuwa baadhi ya watu wamejeruhiwa.


Charamba pia ameliambia gazeti la The Zimbabwe Herald na kusema mlipuko huo ulilenga kumuua Rais Mnangangwa (75) akidai kwamba kumekuwa na mipango ya kumuua ya muda mrefu.


Tukio hilo limetokea saa chache baada ya mlipuko mwingine kutokea wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dk Abiy Ahmed kunusurika kifo alipokuwa akihutubia jijini Addis Ababa. Mlipuko wa Ethiopia umesababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine zaidi ya 100.
Theme images by rion819. Powered by Blogger.