VIJANA 732 WALIOHITIMU MAFUNZO YA JKT KUANZISHA KIWANDA CHA SABUNI KIGOMA

Mkuu wa Kikosi cha KJ 824 Kanembwa wilayani Kakonko Mkoani Kigoma Luteni Kanali Amos Mollo amewapongeza vijana wa oparesheni Mererani waliohitimu mafunzo ya awali ya Jeshi la Kujenga Taifa( JKT  ) kwa andiko walilolifanyia kazi la utengenezaji wa sabuni ambalo litapelekea kuanzishwa kiwanda cha utengenezaji wa sabuni kikosini hapo.

Akizungumza jana wakati wa hafla ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi kwa vijana 732 wanaojitolea yaliyofanyika kwa miezi mitano, Mollo alisema katika kuunga mkono jitihada za Rais wa awamu ya tano wameandaa mpango wa kuanzisha kiwanda cha sabuni za kufulia , kuogea na kunawia mikono ili kuhakikisha falsafa waliyo wafundisha vijana hao ya kujitegemea katika ujasiriamali kwa kuwa vijana hao wamemaliza mafunzo ya awali wataendelea kujifunza stadi za maisha wakiwa kambini hapo.

Alisema anawapongeza vijana hao kwa ujumla kwa kujitolea kuandaa andiko la utengenezaji wa sabuni ambalo wameanza kulifanyia kazi na sasa linaingiza pato kwa Jeshi la Kujenga Taifa ambapo ni matokeo mazuri ya vijana kujifunza na kutumia elimu walioipata ya ujasirimali, uzalendo, kujituma na kujitegemea inayotolewa kambini hapo kuhakikisha vijana wanaondokana na falsafa ya kwamba hakuna ajira jambo ambalo limekuwa wimbo kwa vijana wengi mitaani.

Alisema nje na utengenezaji wa sabuni kikosi hicho kinajihusisha na ukulima wa alizeti, mahindi, kahawa na ufugaji wa nyuki na uchakataji wa asali, ufugaji wa mifugo mbalimbali na utengenezaji wa mafuta ya kupikia ya alizeti lengo ikiwa ni kuwajenga vijana wanaoingia kambini hapo kwa ajili ya mafunzo kuanza kujifunza namna ya ujasiliamali na kujitegemea hata watakapo rudi uraiani wakawe mfano na fundisho kwa vijana wenzao .


Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kuja kujifunza namna ya ujasiriamali kikosini hapo, na kuwataka vijana waliohitimu mafunzo hayo kutumia mafunzo hayo kulinda amani ya nchi na kujishughulisha katika shughuli za maendeleo ili kuondokana na umaskini uliopo katika familia zao.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika sherehe hiyo Mkuu wa wilaya ya Kibondo Louis Bura aliwapongeza wakufunzi wa kikosi hicho kwa kazi kubwa walioifanya ya kuwanoa wahitimu hayo na kuwataka vijana kuyaishi yale mema yote waliojifunza pamoja na mafunzo waliyo yapata waendelee kuonesha nidhamu na utii watakapo endelea kuwepo kambini hapo.

Aidha alimuomba mkuu wa kikosi kuhakikisha anatafuta soko la kuuza bidhaa hizo ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wakurugenzi wa halmashauri kununua sabuni za kusafishia vyoo na kunawia mikono katika kambi hiyo ili kuuunga mkono jitihada za vijana na jeshi la kujenga taifa. 

"Nitoe pongezi zangu za dhati kwa wakufunzi wote najua mnafanya kazi katika mazingira magumu lakini kwa uzalendo mlionao mmehakikisha vijana wetu wanajifunza namna bora ya maisha ikiwa ni pamoja na ujasili, uzalendo wa kujitoa kwa ajili ya nchi yetu pamoja na ujasiliamali hii ndiyo falsafa tuliyoachiwa na waasisi wetu", alisema Bura.

Akisoma risala mbele ya Mgeni rasmi mmoja wa wahitimu hao Deogratius Mgaya alisema mafunzo hayo yamewajenga kuwa wazalendo na walipoanza mafunzo hayo walianza vijana 739 baadhi ya hao walishindwa kumaliza mafunzo yao kwa sababu ya kifo cha mwenzao mmoja na utoro wa baadhi na kupelekea idadi ya waliohitimu kuwa 732 ambao wamepata mafunzo hayo ya awali.

Hata hivyo aliwaomba wazazi kuwahimiza watoto wao kuingia jeshi la kujenga taifa ili kuwafanya vijana kuwa wazalendo na kuepukana na vitendo viovu pamoja na kujijenga katika kutegemea kujiajiri wenyewe na bila kusubili mpaka serikali itoe ajira kwao.
Na Rhoda Ezekiel- Malunde1 blog












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527