MUUGUZI MKUU AKUTWA AMEFARIKI DUNIA SENGEREMA

Muuguzi Mkuu wa Zahanati ya Kijiji na Kata ya Nyakasungwa, Wilayani Sengerema, Mwanza, Grace Mashauri (50) amekutwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake.

Grace alikuwa ni mtumishi pekee aliyekuwa akihudumia zahanati hiyo, ambayo pia haina daktari.

Diwani wa kata hiyo, Feruz Kamizula amesema alipata taarifa hizo leo Mei 28, kutoka kwa watu waliokwenda kupata huduma ya matibabu katika zahanati hiyo baada ya kukosa huduma kwa siku mbili mfululizo.


“Baada ya kupata taarifa hizo leo mchana (jana) nilikwenda katika zahanati hiyo ili kubaini tatizo nilipofika nilikuta mlango wa nyumba umefungwa kwa ndani, lakini baada ya kuzunguka nyuma ya nyumba yake dirishani ilisikika harufu kali,” alisema Kamizula.


Amesema baada ya kubomoa mlango wa nyumba yake walimkuta muuguzi huyo akiwa amefariki dunia.


Mkazi wa kijiji hicho, Esther Kazimili amesema walikwenda Jumamosi Mei 26 katika zahanati hiyo kupata huduma lakini hawakufanikiwa na waliporudi jana hali ilikuwa hivyo hivyo ndipo walipoamua kutoa taarifa kwa diwani huyo.


Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Buchosa, Dk Ernest Chacha amesema ofisi yake imepata taarifa ya kifo cha muuguzi huyo lakini chanzo cha kifo chake hakijafahamika.

“Uchunguzi bado unaendelea na mwili wake umepelekwa hospitali ya wilaya ya Sengerema kuhifadhiwa,” amesema

Naye Mganga Mkuu wa Hospitari teule ya wilaya ya Sengerema Sista Merry Jose amethibitisha kupokea mwili wa marehemu huyo na kwamba umehifadhiwa katika chumba cha maiti na uchunguzi. 

Kamanda wa PolisI Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema hajapata taarifa za kifo hicho huku akiahidi kufuatilia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post