KINANA ANG'ATUKA NAFASI YA UKATIBU MKUU CCM...MWENYEWE AFUNGUKA


Katibu mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameng'atuka nafasi yake aliyokuwa akiishika ndani ya chama hicho na CCM wameridhia ombi hilo rasmi.

Hayo yamewekwa wazi na taarifa zilizotolewa na Katibu wa NEC-Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole leo Mei 29, 2018 na kusema kwa pamoja wamemtakia mafanikio mema katika shughuli zake.

"Napenda kumshukuru ndugu Kinana kwa utumishi wake katika Chama cha Mapinduzi (CCM) na CCM itaendelea kutumia uzoefu wake katika majukumu mbalimbali ya chama kwa kadiri itakavyohitajika", imesema taarifa hiyo.

Kwa upande mwingine, Kinana wakati anatoa neno lake la kuwaaga wajumbe wa NEC amewasisitizia wajumbe hao na wana CCM kiujumla kudumisha umoja wa wanachama na chama cha mapinduzi (CCM).

Kwa upande wake Kinana amesema katika majukumu ya mwanadamu ni lazima kuwe na muda wa kufanya kazi na kupumzika na hakuna jambo lisilo kuwa na mwisho.

Kinana amesema hayo katika kikao cha wa halmashauri kuu Taifa CCM (NEC) katika ukumbi wa mikutano Ikulu Jijini Dar es salaam wakati wa kutangaza kustaafu nafasi ya Ukatibu Mkuu wa chama hicho na kuongeza kuwa anashukuru wanachama na viongozi wa chama hicho kwa ushirikiano kwa kipindi cha uongozi wake.

“Lazima tukubali kuna wakati wa kufanyakazi na wakupumzika, naelewa ugumu mnaoupata wa kutokunikubalia, tumekuwa na makatibu wakuu saba kwahiyo sio ajabu katibu mkuu wa sasa kuanchia ngazi ili apatikane mwingine, nashukuru mwenyekiti, makamu mwenyekiti na mzee Mangula kwa kunikubalia na kutambua kuwa kila lenye mwanzo lazima liwe na mwisho”, amesema Kinana.

Kinana ameongeza kuwa amepokea simu na ujumbe mwingi katika simu yake za wanachama na viongozi wa chama hicho wakimtaka kuendelea na nafasi ya ukatibu mkuu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527