ASKOFU WA KKKT ALIYEPIGWA MAWE AIBIWA KITI

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Njombe, Isaya Mengele, amesema kuwa kitendo kilichofanywa na baadhi ya waumini wa kanisa hilo Dayosisi ya Ziwa Tanganyika kumjeruhi kwa kumpiga mawe Askofu wa KKKT Dayosisi ya Tanganyika, Ambele Mwaipopo,limelitia doa kanisa hilo na kinapaswa kulaaniwa.


Akizungumza jana katika ibada maalum iliyofanyika katika Kanisa la Kiaskofu la KKKT Usharika wa Sumbawanga Mjini, Askofu Mengele ambaye ni Mwenyekiti wa maaskofu wa KKKT Kanda ya Kusini, alisema ni aibu kubwa na fedheha kwa dayosisi hiyo yenye miaka minne tangu kuanzishwa kwake na waumini hao wanapaswa kutubu na kuomba radhi.


Alisema kuwa pia yeye ataongoza ujumbe wa maaskofu wa kanda hiyo kwenda kwa Rais John Magufuli kumuomba radhi kwa kitendo cha baadhi ya waumini hao kuvuruga amani ambayo serikali yake imekuwa ikiihimiza kwa kitendo cha kumjeruhi kwa kumpiga mawe Askofu Mwaipopo.


Pia Askofu alimshauri Askofu Mwaipopo kuvunja Baraza la Dayosisi hiyo kwa kuwa baadhi ya wajumbe wake wamekuwa ni chanzo cha mgogoro uliopo katika kanisa hilo na wamekosa utii kwake.


Muda mfupi kabla maaskofu sita wanaounda Kanda ya Kusini ya KKKT hawajafika kuongoza ibada ya jana na kumpa pole Askofu Mwaipopo kwa kujeruhiwa, baadhi ya waumini waliingia katika kanisa hilo na kuondoa kiti maalum cha kukalia askofu huyo wakati wa kuongoza ibada.


Maaskofu hao ni Renald Mtenji wa Ulanga Kilombero, Askofu Blastone Gaville (Dayosisi ya Dira-Iringa), Askofu Job Mbwilo (Dayosisi ya Kusini Magharibi- Matamba), Askofu Amon Mwenda (Dayosisi ya Ruvuma), Askofu Edward Mwaikali (Dayosisi ya Konde Mbeya) na Askofu Isaya Mengele (Dayosisi ya Kusini Njombe).


Lengo la jopo hilo la maaskofu hao limefika kumpa pole Askofu Mwaipopo na kuwasihi waumini waache mara moja vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuwa vinaliumiza na kulichafua kanisa hilo ambalo lina zaidi ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake nchini.


Katika ibada hiyo Katibu wa Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Fredrick Lazaro, alisoma tamko maalum la Halmashauri Kuu kwa wakristo wa Usharika wa Kathedral Sumbawanga Mjini kuekeleza waumini 21 na watumishi wa kanisa hilo kuwa wamejitenga na kanisa hilo kwa muda usiojulikana.


Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Alfan Haule, alisema vitendo vya uvunjifu wa amani havitafumbiwa macho na serikali na kama vitaendelea, itatumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuvidhibiti.


Dk. Khaule aliagiza kuwa wote walioiba kiti cha Askofu Mwaipopo wasakwe na wakamatwe, ili wafikishwe mbele ya sheria wachukuliwe hatua kwani kitendo cha kuiba kiti hicho ni wizi kama wizi mwingine wowote.


Mei 7, mwaka huu, Askofu Mwaipopo alifukuzwa kwa mawe baada ya baadhi ya waumini kumzuia kuingia usharikani wakidai hawataki kumuona akiwepo eneo la kanisa la Usharika wa Simbawanga Mjini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527