WAZIRI MKUU AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUPIGANIA AMANI YA NCHI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini popote walipo wahakikishe wanaipigania na kuilinda amani kwa kila hali ikiwa ni pamoja na kupambana na viashiria vya uvunjifu wa amani.


Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Machi 31, 2018) kwenye Mkutano Mkuu wa BAKWATA uliofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa ni muhimu wasaidizi wa Mufti wakasimamia suala hilo.


“Dini ni taasisi muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku ndio maana Serikali inaheshimu na kuzitambua dini zote kutokana na mchango wake mkubwa katika amani ya nchi yetu. Niwaombe viongozi wangu popote mlipo muilinde amani yetu”


Waziri Mkuu amesema amani ni miongoni mwa neema kubwa sana kwa binadamu na ndio maana wote wanamtambua Mwenyezi Mungu, hivyo wasiruhusu mtu au kikundi chochote kujaribu kuchafua na kuharibu amani iliyopo nchini.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wahakikishe kuwa chombo hicho kinaendelea kuwaunganisha waislamu bila ya kujali makabila yao, rangi zao au madhehebu yao.


Waziri Mkuu amesema Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar bin Zubeiry ambaye ndiye kiongozi wa Waislamu nchini mara zote amekuwa akisisitiza jambo hilo na kuwataka waislamu popote walipo watambue kuwa hicho ni chombo chao.


“Ni muhimu sana kwa ninyi wasaidizi wa Mufti mlio kusanyika hapa muhakikishe mnalisimamia hili katika maeneo yenu. Katika hili napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yenu iko pamoja Mheshimiwa Mufti kutekeleza nia hiyo njema.”


Amesema ahadi ya Rais Dkt. Magufuli ni kuwa Serikali anayoiongoza ipo tayari kusikiliza maoni, ushauri na mapendekezo yeyote kutoka kwa viongozi wa dini . ‘Milango iko wazi saa zote ‘


Ameongeza kuwa yeye si mtaalamu sana kama walivyo Masheikh hao lakini anakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’ani sura Al Imran aya ya 103 yanayosema “ Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote na wala msifarakane”


Mkutano huo umehudhuriwa na Sheikh Mkuu wa Mufti wa Tanzania Sheikh Zubeir, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Masheikh na viongozi wa BAKWATA wa mikoa na wilaya zote Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527