WAZIRI MHAGAMA : SERIKALI HAITAPUUZA USALAMA NA AFYA ZA WAFANYAKAZI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mh. Jenista Mhagama, akisalimiana na watumishi wa OSHA mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Kichangani mjini Iringa ambako maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi Duniani yalifanyika. Aliombatana nao ni Katibu Mkuu katika Wizara yake, Eric Shitindi na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda.
 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mh. Jenista Mhagama, akiwa katika banda la OSHA katika maonesho ya Usalama na Afya mahali pa kazi yanayofanyika katika viwanja vya Kichangani mjini Iringa. Alioongozana nao ni Katibu Mkuu katika Wizara yake, Eric Shitindi na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda. 

*****
Serikali imesema kamwe haitapuuza suala la Usalama na Afya mahali pa kazi hususani katika kipindi hiki ambacho msisitizo mkubwa ni katika kujenga uchumi wa viwanda.

Msimamo huo wa serikali umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mh. Jenista Mhagama, alipokuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Iringa na wageni mbali mbali waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi Duniani.

Mh. Mhagama ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa maadhimisho ya siku hiyo ambayo huadhimishwa kila ifikapo Aprili 28, alisema katika kipindi hiki ambapo mwelekeo wa nchi ni kujenga uchumi wa viwanda, suala la usalama na afya za wafanyakazi ni lazima lizingatiwe.

“Ningependa kusisitiza kuwa, serikali ya awamu ya tano kamwe haitapuuza suala la usalama na afya mahala pa kazi hasa wakati huu tunapojenga uchumi wa viwanda ambao utaambatana na vihatarishi vingi vipya,” alisema Mh. Waziri na kuongeza: 

“Kwa hivyo, itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kupunguza au hata ikiwezekana kuondoa kabisa vifo, ajali, magonjwa na madhara yatokanayo na kazi”.

Kwahapa nchini, masuala ya Usalama na Afya katika sehemu za kazi, yapo chini ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ambao husimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Bunge ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

OSHA husajili sehemu zote za kazi nchini na kuzitembelea kwaajili ya kufanya kaguzi za kiusalama na afya ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na mifumo madhubuti ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi mbali mbali vitokanavyo na kazi wanazozifanya.

Na Eleuter Mbilinyi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post