RAMAPHOSA AONGOZA MAELFU YA WANANCHI KUMZIKA WINNIE MANDELA


Johannesburg, Afrika Kusini. Rais Cyril Ramaphosa pamoja na watangulizi wake Jacob Zuma na Thabo Mbeki walikuwa miongoni mwa maelfu ya wananchi waliohudhuria mazishi ya mpigania uhuru, Winnie Madikizela Mandela yaliyofanyika kitaifa Jumamosi katika Uwanja wa Orlando, Soweto.


Mwili wa Winnie Mandela ulitarajiwa kupelekwa kwa maziko kwenye makaburi yaliyopo kitongoji cha Fourway umbali wa kilomita 40 Kaskazini mwa Soweto.


Waombolezaji waliimba sifa za Winnie wakati jeneza lenye mwili wa mwanamama huyo shujaa lilipokuwa likiingizwa kwenye uwanja huo umbali wa chini ya kilomita mbili kutoka nyumbani kwake.


Jeneza lake lilifunikwa kwa bendera ya Afrika Kusini na baada ya kuingizwa liliwekwa katikati ya uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 37,500 wote wakiwa wamekaa.


Waombolezaji walikuwa wamevaa mavazi ya rangi za chama tawala cha African National Congress (ANC), na za chama cha upinzani chenye siasa kali cha Economic Freedom Fighters (EFF), huku wakiimba “hakuna, hakuna kama Winnie”, wimbo maarufu kutoka enzi za harakati za ukombozi.


Mazishi hayo yamehitimisha siku 10 za maombolezo ya kitaifa kipindi ambacho maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini walitoa heshima zao kwa “Mama wa Taifa” nyumbani kwake Soweto na kwingineko.


Winnie Mandela, aliyefariki dunia katika hospitali jijini Johannesburg akiwa na umri wa miaka 81, Aprili 2 baada ya kuugua muda mrefu, amepongezwa kwa kusaidia kuweka hai ndoto ya Nelson Mandela ya Afrika Kusini kuwa nchi isiyo ya ubaguzi wa rangi wakati yeye akiwa gerezani kwa miaka 27.


“Alikuwa mmoja wa viongozi jasiri katika chama cha ANC,” alisema mwombolezaji Brian Magqaza, 53. “Alipambana kuanzia mwanzo hadi mwisho. Nenda Mama yetu nenda.”


Mfuasi wa EFF Mufunwa Muhadi, 31, alisema “Mama alipigania uhuru wetu. Ni muhimu sana kumpa heshima na tundeleze mapambano”.


Rais Cyril Ramaphosa, aliyeingia madarakani miezi miwili iliyopita, aliongoza waombolezaji katika misa iliyofanyika kwenye uwanja huo wa Orlando.


Marais wa zamani Jacob Zuma na Thabo Mbeki pia walishiriki. Lakini waombolezaji bila kujali huzuni zao walimzomea Zuma alipotangazwa kutambua uwepo wake.


Watu kadhaa mashuhuri kutoka nje walihudhuria wakiwemo viongozi wa Namibia, Swaziland na Jamhuri ya Congo, pamoja na mwanaharakati wa haki za binadamu Jesse Jackson wa Marekani. “Huyu ni mama halisi wa Afrika Kusini,” Jackson aliwaambia wanahabari.
 Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527