Thursday, April 26, 2018

NDEGE KUBWA YA EMIRATES ILIYOTUA DAR NI BALAA..INA GHOROFA..NI KAMA HOTELI KIFAHARI

  Malunde       Thursday, April 26, 2018

 Unaweza kufananisha baadhi ya maeneo kwenye ndege ya Airbus A380-800 ya kampuni ya Emirates iliyotua kwa dharura jijini Dar es Salaam na vyumba vya kifahari vya hoteli.


Na si tu vyumba, bali huduma zinazotolewa ndani ya ndege hiyo iliyoondoka jana ni za kifahari mithili ya hoteli kubwa za nyota tano.

Ndege hiyo ilitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jumatatu baada ya kushindwa kutua Mauritius kutokana na mvua. Iliondoka jana saa 2:15 asubuhi kuendelea na safari ya Mauritius.

Ndege hiyo ya kifahari ya ghorofa, ina ukumbi wa starehe (lounge), kaunta; huduma ya kusinga (massage) na intaneti isiyo ya waya (Wi-Fi).

“Pata matukio makubwa ya moja kwa moja pamoja na wasafiri wenzako kwa kutumia skrini ya inchi 55 ya televisheni ya LCD na sauti yake unajisikia uko kwenye tukio,” inasema tovuti ya Emirates kuhusu huduma za ndege hiyo.

Tovuti hiyo pia inaeleza kuwa ndani kuna eneo la kujirejeshea nguvu na kujisikia mpya kwa kukandwakandwa (massage) na kutumia mafuta kabla ya kutua sehemu unayotaka.

Tovuti hiyo inaeleza kuwa abiria wa daraja la kwanza wanaweza kukunjua viti na kuwa kitanda kamili, huku mteja akiwa huru kuchukua kinywaji chochote atakacho kutoka kwenye friji ndogo iliyo pembeni yake.

Mbali na huduma hizo, abiria wa daraja la kwanza wanaweza kujifungia iwapo wanataka faragha ya kutowasiliana na wengine.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa alisema jana wakati wa kujibu michango ya wabunge kuwa ndege hiyo iliyokuwa inatokea Dubai ina uwezo wa kubeba abiria 868 na juzi ilikuwa na abiria 503.

“Baada ya kufika kisiwa cha Madagascar walipata taarifa kwamba hali ya hewa Mauritius ni mbaya, kwa kawaida ukipata taarifa hiyo unakwenda uwanja wa ndege uliopo karibu,” alisema.

Hata hivyo, kuna vigezo vinginevyo vya ndege kutua kwa dharura ikiwa ni pamoja na fomu maalumu ambayo marubani hujaza wakieleza endapo kutatokea dharura uwanja gani watue.

Pia, ukaribu kutoka eneo la dharura na alipo, uwepo wa huduma muhimu kama vile hoteli za nyota tano au nne za kulaza abiria, huduma za afya na uwanja kutokuwa na shughuli nyingi.

Taarifa kutoka ofisi za Emirates Tanzania zilisema abiria wa ndege iliyotua kwa dharura walilala katika hoteli za Holiday Inn, Colloseum, Serena, Hyatt Regency, Ramada Encore, New Africa na Golden Tulip.

Na Elias Msuya na Fidelis Butahe mwananchi
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post