MAMIA YA WANAWAKE WALIOZALISHWA WAJAZANA OFISI ZA MAKONDA


Mamia ya wanawake waliotelekezwa baada ya kuzalishwa na waume zao wamejazana katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyetangaza kuanza kuwasikiliza.

Kumekuwa na mafuriko ya wanawake wanaoingia kwa kusukumana kwenye ofisi hizo hali iliyowalazimu walinzi kufunga geti ili walio ndani wahudumiwe.

Wanasheria na wafanyakazi wengine wa ofisi hiyo wanaendelea kuwasikiliza wanawake hao wengi wao wakiwa wamebeba watoto wao.

Wakizungumza  leo, Aprili 9 wanawake hao wamesema wingi wao unaweza kusababisha baadhi yao kushindwa kusikilizwa.

"Nilitelekezwa na watoto wanne kwenye nyumba ya kupanga, nimekuwa kama ombaomba nashukuru Makonda ameona kilio chetu lakini kwa umati huu naogopa sana,"amesema mwanamke mmoja.

Wapo waliolala kwenye ofisi hizo huku wengine wakianza kuwasili tangu saa tisa za usiku.

Vimetengwa vyumba maalum zikiwamo kumbi zilizo katika ofisi hizo kwa ajili ya kusikiliza kilichowasibu wanawake hao.

Na Tumaini Msowoya, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527