AKAMATWA NA POLISI KWA KUIBA MALI ZA MSIKITI MOROGORO

Ally Ngolo anashikiliwa na polisi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kuiba mikeka, mbao na baiskeli ambavyo vyote ni mali ya msikiti wa Masjid Nuru kichangani, Manispaa ya Morogoro.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Aprili 4, 2018 katibu wa msikiti huo, Sheikh Kudra Milonge amesema kuwa Ngolo alifika katika msikiti huo mwezi mmoja uliopita akiwa na mke wake pamoja na watoto wawili kwa madai kuwa wamekuja kubadili dini.


Amesema baada ya kubadili dini alidai hana uwezo wa kujikimu kimaisha, hivyo waumini wa msikiti huo waliamua kumchangia fedha na kumpa chumba kimoja kwenye nyumba ya imamu.


Amesema waumini walimnunulia mtu huyo godoro pamoja na vyombo vya kupikia pamoja na kumpa mradi wa kuuza maji msikitini hapo.


Sheikh Milonge amesema baada ya kuishi kwa mwezi mmoja, Machi 26 mwaka huu aliiba vitu hivyo na kutoweka na familia yake.


Mweka Hazina wa msikiti huo, Mohamed Hussein amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa kwenye msikiti wa kiwanja cha ndege Manispaa ya Morogoro akiwa kwenye harakati za kufanya utapeli huo.


Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amethibitisha kukamatwa kwa mtu huyo na kwamba uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.


Na Hamida Shariff, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527