AFISA KILIMO AJIUA KWA KUNYWA SUMU NA KUJINYONGA NDANI YA ZIZI LA NG'OMBE


Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Michael Fundo (57), amefariki dunia kwa kunywa sumu kabla ya kujitundika kwa kamba ndani ya zizi la ng’ombe nyumbani kwake wilayani Misungwi mkoani Mwanza.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo linalodaiwa kusababishwa na msongo wa mawazo kutokana na Michael kuwa na ugomvi wa muda mrefu wa kifamilia.


Mmoja wa wanafamilia aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, amesema ugomvi huo ulitingisha pia ndoa yake.


“Kabla ya kujinyonga kwa kamba, alikunywa sumu aliyoona inamchelewesha,” amesema Kamanda Msangi.


Licha ya kuwa mtumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Nyamagana ambayo kwa pamoja na Ilemela zinaunda Jiji la Mwanza, Michael alikuwa akiishi wilaya jirani ya Misungwi.


Mtumishi wa ndani wa familia hiyo, John Anthony (23) amesema kabla ya kuchukua uamuzi wa kujitoa uhai, alifanya hesabu ya kikundi cha kuweka na kukopa ambacho alikuwa mtunza fedha na kukabidhi nyaraka na fedha zote akielekeza zikabidhiwe kwa wana kikundi wenzake.


“Marehemu pia aliandika waosia ukihusisha mali pamoja na madeni anayodai na kudaiwa, jambo lililotutia mashaka ni kwa nini anafanya hivyo,” amesema Anthony.


Kwa mujibu wa mmoja wa wanakikundi, leo Aprili 28, walipanga kugawana fedha walizokusanya.


Na Twalad Salum, Mwananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527