ZITTO KABWE KUPAMBANA NA POLISI TANZANIA


Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo, Kabwe Ruyagwa Zitto amefunguka na kusema kuwa chama chake tayari kimefungua kesi ya Kikatiba katika mahakama Kuu Dar es Salaam kulishtaki jeshi la polisi.

Zitto Kabwe amesema hayo leo Machi 18, 2018 wakati akitoa tathmini ya ziara alizofanya kutembelea Madiwani katika kata mbalimbali nchini zinazoongozwa na ACT Wazalendo ambapo amedai katika ziara hiyo wamebaini mambo mengi ikiwa pamoja na hali ya maisha kuwa ngumu sana, migogoro ya ardhi, kukosekana kwa huduma ya Maji safi na salama, ukosefu wa huduma bora za afya, tatizo la Miundombinu ya Usafirishaji.

Kiongozi huyo aliendelea kuweka wazi mambo mbalimbali ambayo wamefanikiwa kuyaona katika ziara hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa pembejeo za Kilimo, ukosefu wa masoko ya mazao ya wavuvi, wakulima na wafugaji, kushuka kwa bei ya mazao yao, kupanda kwa gharama za maisha ya watu, kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi, upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, vyoo pamoja na walimu, na kuzorota kwa hali ya usalama wa wananchi pamoja na mali zao, hali mbaya ya ajira kwa vijana pamoja na uminywaji mkubwa wa demokrasia na uhuru wa watu kukusanyika na kujieleza.

"Tumefungua Kesi ya Madai Na. 8/2018 Mahakama Kuu hapa Dar Es Salaam, kulishtaki Jeshi la Polisi, kutokana na Jeshi hilo kuingilia, visivyo halali shughuli, ziara yetu ya kuhamasisha maendeleo katika Kata tunazoziongoza. Tunaamini Mahakama itatenda haki kwenye suala hili"alisema kiongozi huyo 

Aidha Zitto Kabwe ametoa ushauri kwa serikali kuhusu suala la Demokrasia nchini na kusema kuwa mazungumzo ya kitaifa ndiyo yanaweza kuwa na jibu kuhusu masuala haya na kuleta utatuzi juu ya jambo hili. 

"Demokrasia na Ustawi wa Taifa tunaendelea kusisitiza rai yetu kuhusu umuhimu wa kuitisha Mkutano wa Kitaifa wa maridhiano ya kisiasa kama jukwaa la kuzijadili changamoto za uendeshaji wa siasa nchini. Jambo hilo litaondoa uadui unaoendelea kukua sasa kati ya serikali na wananchi, viongozi wa dini, mashiriki yasiyo ya Kiserikali, taasisi za wanafunzi, pamoja na vyama vya Upinzani. Tunaamini mazungumzo ya Kitaifa ndio jambo sahihi la utatuzi wa suala hili" alisisitiza Zitto Kabwe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527