Friday, March 2, 2018

Picha : MGODI WA BULYANHULU WAKABIDHI MRADI WA MAJI NA UZIO WA SHULE KAKOLA KAHAMA

  Malunde       Friday, March 2, 2018
Kampuni ya Uchimbaji madini ya Acacia kupitia Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu (BGML) imekabidhi mradi wa maji kwa wananchi wa kijiji cha Kakola na mradi wa uzio wa shule kwa shule za msingi Kakola A na B zilizopo katika kijiji na kata ya Kakola halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga.


Miradi hiyo iliyojengwa na wakandarasi wazawa iliyogharimu jumla ya shilingi milioni 334.9 zilizotolewa na Acacia imekabidhiwa leo Ijumaa Machi 2,2018 na uongozi wa mgodi wa Bulyanhulu kwa Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala,Leonard Mabula.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo,Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu,Jon Almond ujenzi wa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa program za kuchangia maendeleo ya jamii ili kuboresha miundombinu ya jamii na kiuchumi kwenye maeneo yaliyo jirani na migodi.

Alisema mgodi huo umegharamia uwekaji wa uzio “Fence”,yenye urefu wa kilomita 1.28 kwenye shule hizo mbili kwa shilingi milioni 145.2 kwa kutumia mkandarasi PKM Ltd kutoka mkoa wa Mara.

Aidha Almond alisema mgodi huo pia umegharamia shilingi milioni 189.6 katika ujenzi wa mradi wa maji ya kisima kirefu ikiwemo kuunganisha pampu ya umeme ya kuvuta maji na ujenzi wa mnara wa matanki matano kila moja likiwa na ujazo wa lita 10,000.

Aliongeza kuwa ujenzi huo wa mradi wa maji umetekelezwa na wakandarasi kadhaa wakiwemo HI-GEN Construction Ltd wa Kahama,ENIKON Ltd wa Mwanza na Namwahi Ltd wa Geita.

 “Leo tuna furaha kubwa kukabidhi miradi hii,mradi wa maji utawanufaisha zaidi ya wananchi 3000 waliokuwa na changamoto ya maji na uzio huu utasaidia kuweka mipaka ya shule katika hali ya usalama na wanafunzi zaidi ya 4000 kuwa katika mazingira tulivu na walimu kufuatilia mienendo ya wanafunzi wanaotoka na kuingia shuleni”,alieleza Almond.

“Utekelezaji wa miradi hii umefanikiwa kwa urahisi kutokana na ari ya ushirikiano na mahusiano mazuri kati ya mgodi ,wananchi na serikali na kinachofurahisha zaidi ni kwamba miradi hii ilipendekezwa na wananchi wenyewe kupitia uongozi wa kijiji kama miradi ya kipaumbele”,aliongeza Almond.

Alibainisha kuwa kumalizika kwa mradi wa maji kunachangia kwenye kipengele cha 10 cha dira ya maendeleo ya Tanzania ifikapo mwaka 2025 inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwenye maeneo ya vijijini kufikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2020/21 na kwa upande wa uzio wa shule ni nyongeza ya miradi mbalimbali ya Acacia kusaidia sekta ya elimu.

Akizungumza wakati wa kupokea miradi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya MsalaLa,Leonard Mabula aliushukuru mgodi huo kwa kuendelea kushirikiana na jamii katika kuwaletea maendeleo na kuwataka wananchi kutunza miradi hiyo ili iwe endelevu.

“Acacia wametupunguzia adha ya maji katika eneo hili,naomba wananchi mlinde mradi huu ili uwe endelevu lakini pia tuutunze uzio huu,uongozi wa kijiji fanyeni vikao na mikutano mkubaliane namna ya kulinda uzio huu na mpange bei nzuri ya maji kwa kila mwananchi kuimudu”,aliongeza.

Mabula alisema pamoja na Acacia kuendelea kuisaidia jamii ya Kakola kwa kuwekeza katika miradi ya maendeleo ikiwemo ya maji,huduma za afya,elimu,kilimo,michezo,umeme na miundo mbinu aliomba mgodi kuendelea kusaidia wananchi.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Jon Almond akizungumza wakati wa kukabidhi mradi wa maji na uzio wa shule kwenye shule za Msingi Kakola A na B katika kijiji cha Kakola kata ya Kakola halmashauri ya Msalala - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala,Leonard Mabula akizungumza wakati wa kupokea miradi ya Maji na uzio katika shule za msingi Kakola A na B.
Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Leonard Mabula akimpongeza Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Jon Almond kwa kusaidia ujenzi wa miradi mahsusi ya maji na uzio katika kijiji cha Kakola na kuomba Acacia kuendelea kushirikiana na jamii katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Katikati ni Afisa Mawasiliano mgodi wa Bulyanhulu Mary Lupamba akitoa maelekezo kabla ya zoezi la kukata utepe wakati wa uzinduzi wa uzio 'fence' katika shule za msingi Kakola A na B zilizopo katika kijiji cha Kakola kata ya Kakola halmashauri ya Msalala.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Leonard Mabula akikata utepe kuzindua uzio 'fence' katika shule za msingi Kakola A na B. Nyuma yake ni Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Jon Almond.
Bango likisomeka "Mradi wa uzio wa shule ya msingi Kakola A na B umefadhiliwa na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu". Uzio huo umefunguliwa na Leonard Mabula kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Simon Berege.
Muonekano wa sehemu ya 'fence' uzio huo.
Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Jon Almond akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Leonard Mabula wakielekea katika mradi wa maji ya kisima kirefu katika kijiji cha Kakola kwa ajili ya kuufungua. 
Eneo la mradi wa maji ya kisima kirefu katika kijiji cha Kakola.
Zoezi la uzinduzi/ufunguzi wa mradi wa maji likiendelea.
Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Jon Almond akishikana mkono na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Leonard Mabula wakati wa kufungua mradi wa maji katika kijiji cha Kakola.
Mradi wa Maji Kakola umefadhiliwa na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu. Mradi huo umefunguliwa na Leonard Mabula kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Simon Berege.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Leonard Mabula na Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Jon Almond na wakiwa wameshikilia glasi za maji wakijiandaa kuchota maji na kunywa wakati wa kufungua mradi wa maji.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Leonard Mabula na Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Jon Almond wakinywa maji katika mradi wa maji Kakola wakati wa kufungua mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Leonard Mabula akimtwisha ndoo ya maji Hadija Ponsiano wakati wa kufungua mradi wa maji Kakola.
Wakazi wa Kakola wakipata huduma ya maji baada ya mradi kufunguliwa. Kulia ni Edina Fedrick akipokea pesa kwa mwananchi aliyefika katika mradi huo kununua maji yanayouzwa kwa gharama nafuu.
Mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Kakola A, Nandula Samson akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wa shule za msingi Kakola A na B. Alisema wanaishukuru Acacia kwa kuwajengea uzio na sasa watakuwa katika mazingira salama zaidi.Alieleza kuwa shule hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.
Kushoto ni Kaimu Meneja Uhusiano na Ufanisi mgodi wa Bulyanhulu,katikati ni Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Jon Almond akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala, Leonard Mabula wakisikiliza risala ya wanafunzi wa shule za msingi Kakola A na B.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Kakola,Daud Simon akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya miradi ya uzio wa shule na maji katika kijiji cha Kakola.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kakola Emmanuel Bombeda akizungumza wakati makabidhiano ya miradi ya uzio wa shule na maji katika kijiji cha Kakola.
Waigizaji kutoka kundi la Nuru kutoka Kakola wakiigiza namna changamoto ya maji inavyotesa jamii.
Wanafunzi wa shule ya msingi Kakola B,waliovaa masweta ya bluu wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea.
Wanafunzi wakiwa wamesimama. Waliovaa masweta ya kijani ni wanafunzi wa shule ya msingi Kakola A, waliovaa masweta ya bluu ni wanafunzi wa shule ya msingi Kakola B.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post