MLINZI SUMA JKT AUAWA KWA KUKATWA MAPANGA


JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema watu wasiojulikana wamemvamia mlinzi wa SUMA JKT Chewe Wilson(34) na kumsababisha kifo baada ya kumkata mapanga sehemu za kichwani na mguu na kisha kupora silaha yake akiwa lindoni.

Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Mohamed Mpinga amesema kuwa jeshi hilo limeendelea na jitihada zake za kukabiliana na matukio ya uhalifu ambapo kwa siku kadhaa sasa limekuwa likiendelea kufanya msako kwenye maeneo mbalimbali.
Kamanda Mpinga amesema kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa usalama, jeshi hilo limepata mafanikio makubwa katika kudhibiti wahalifu na matukio ya uhalifu mkoani Mbeya.

"Tumefanikiwa kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kukamata watuhumiwa mbalimbali wa uhalifu, silaha na vifaa mbalimbali vya kutengenezea silaha,"amesema.

MLINZI SUMA JKT AUAWA KIKATILI

Kamanda Mpinga amesema usiku wa kuamikia Februari 26 mwaka huu huko maeneo ya Kituo cha mafuta kiitwacho Manyanya kilichopo Uyole jijini Mbeya watu wasiofahamika majina walimvamia mlinzi wa SUMA JKT aitwaye Chewe Wilson mkazi wa Iduda.
"Mlinzi huyo akiwa lindoni katika kituo hicho alivamiwa na kisha kukatwa mapanga na silaha aliyokuwa nayo ikaporwa na watu hao na baada ya hapo wakatoroka nayo,"amesema Kamanda Mpinga.

Amefafanua mlinzi huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kutokana na majeraha aliyoyapata sehemu za kichwani.

Kamanda Mpinga amesema kutokana na tukio hilo Polisi walifanya msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano ambao baada ya kuhojiwa wamekiri kuhusika na tukio hilo.

"Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara baada ya upelelezi kukamilika,"amesema.


WADAKWA WAKIWA NA GOBORE
Kamanda Mpinga amesema wamefanya msako katika Kitongoji cha Kibaoni wilayani Chunya na kuwakamata watu wawili wakiwa na bunduki aina ya Shortgun iliyotengenezwa kienyeji na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengenezea bunduki.

Amewataja watuhumiwa hao ni Fadhili Mayega(60), na Mashaka Samuel(38), wote wakazi wa Kambikatoto

Ameongeza baada ya watuhumiwa kupekuliwa walikutwa na bunduki hiyo na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengenezea bunduki aina ya shortgun za kienyeji ambavyo ni mkono wa kuwekea risasi kwenye bunduki, unga wa baruti wenye uzito wa gramu moja.
Pia mafuta ya kusafishia bunduki, risasi 25 zilizotengenezwa kienyeji, tupa 10, chuma kimoja cha kukatia risasi, tindo za kukatia mawe, vipande vya vyuma viwili, visu vitano, nyundo kubwa mbili, bisibisi moja, mguu wa Pedal ya baiskeli na triger mbili.

"Watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara tu baada ya upelelezi kukamilika,"amesema Kamanda Mpinga.

Ametoa mwito kwa vijana na jamii kwa ujumla kuacha tamaa ya kupata mali kwa njia zisizo halali kwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwani ni kinyume cha sheria na badala yake wajishughulishe na kazi halali kwa ajili ya kujipatia kipato.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527