Friday, March 9, 2018

MAMIA WAJITOKEZA KUMZIKA MWANASIASA MKONGWE DKT. KABOUROU KIGOMA

  Malunde       Friday, March 9, 2018
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga amewaongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Kigoma, viongozi wa serikali, vyama vya siasa katika mazishi ya Mwanasiasa Mkongwe na Mwenyekiti msaafu wa Chama cha Mapinduzi mkoani Kigoma, Dkt. Amani Kabourou.

Mazishi yamefanyika leo Ijumaa Machi 9,2018 nyumbani kwa mama yake Ujiji Buzebazeba katika Makaburi ya Kipampa.

Akizungumza katika msiba huo, Mkuu huyo alisema Kabourou ni mwanasiasa Mkongwe aliyetetea haki ya wana Kigoma na alikuwa wa kwanza kutetea mkoa huo na kupambana kupatikana kwa maendeleo mkoani humo ili kuhakikisha kila mwanakigoma anapata haki yake.

Alisema serikali na chama kitakumbuka mchango mkubwa wake alioufanya mkoani Kigoma na kwamba anatakiwa kuigwa kwa uongozi alioufanya ameacha alama kwa kuwa kiongozi mpenda haki na alifanya kazi bila ubaguzi wa chama wala dini.

"Marehemu atakumbukwa kwa mchango wake na alipokuwa kiongozi wa vyama mbalimbali na hata katika Bunge la Afrika Mashariki alikuwa mwanamageuzi kutokana na usomi aliokuwa nao",

 "Wanasiasa na siasa ya mkoa wa Kigoma tutamkumbuka kwa wkua ndiye aliyeleta chachu ya wanasiasa wa mkoa na vijana wote wanasiasa ni wanafunzi wa Kabourou na kwa kipindi hiki tujitahidi kuyaishi mazuri yake aliyoyafanya kwa kipindi alichokuwa kiongozi na kuyatendea kazi", alisema mkuu huyo.


Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma Amandusi Nzamba alisema Chama kimepata pigo kubwa sana kumpoteza Mwanasiasa huyo kwa kuwa ni mwanasiasa aliyesaidia chama hicho kwa sehemu kubwa na mpaka sasa chama hicho kimejengwa katika misingi mizuri na wanakigoma wataendelea kuukumbuka mchango wake.

Alisema chama hicho kitaendelea kumkumbuka Kabourou kwa kuwa ni kiongozi shupavu na aliyekuwa akijituma na akijitoa kikamilifu katika chama na kuwaomba wanachama na viongozi wote kuiga nyao za kiongozi huyo ili kuweza kukipeleka mbele chama hicho.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la kigoma Mjini Zitto Kabwe alisema kama mtoto na mwanafunzi wa Kabourou pamoja na tofauti za kisiasa ndiye aliyekuwa mwalimu wao na aliyewazibua masikio na wote wamepita alikopita Kabourou.

 Alisema Kabourou alifundisha wengi na jukumu kubwa ni kuhakikisha umoja na mshikamano kupeleka mbele maendeleo ya wanakigoma.

"Ni Kiongozi wa kwanza kupitia mfumo wa vyama vingi aliyejitoa kupambana na kupigania siasa mkoani Kigoma na kwamba ni Kiongozi atakayekumbukwa na wanaKigoma wote kwa kazi kubwa aliyoifanya na kwa kumuenzi wataendelea kuiga nyayo za kiongozi huyo.

Mwenyekiti wa BAKWATA mkoani Kigoma Salim Kangeta alisema Kabourou ni Kiongozi aliyekuwa akishirikiana na kila mtu na hata viongozi wa dini na alikuwa anasikiliza ushauri kwa mtu yeyote kuhakakikisha Kigoma inasonga mbele na ni kiongozi aliyesababisha muamko wa viongozi wa vyama vya upinzani kujiamini mkoani Kigoma na ni kiongozi aliyeisaidia CCM kuongeza majimbo hata katika wakati wa uongozi wake kama Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma.


Marehemu alizaliwa Mwaka 1949 Mkoani Kigoma alisoma elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Kipampa na elimu ya sekondari katika shule ya Living stone Kigoma na baada ya hapo aliondoka na kwenda kuendelea na masomo yake Nchini Marekani ambapo baada ya hapo alirejea nchini na kuanza harakati za siasa ambapo alianza kuwa mbunge wa jimbo la Kigoma kwa kipindi cha miaka tisa, aliwahi kuwa mbunge wa bunge la Afrika mashariki, katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema Tanzania bara na amewahi kuwa Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Mkoani Kigoma.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blogUsikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post