MAGARI 13 KUSHIRIKI MBIO ZA MAGARI "MKWABI TANGA RALLY 2018" MKOANI TANGA


Mratibu wa Mashindano ya Magari  Tanzania,Faheem Ao akizungumza na wandishi wa habari kuhusiana na  Mashindano hayo wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari 
Mkoani Tanga Akida Machai
Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari Mkoani Tanga Akida Machai kulia akizungumza kuhusiana na mashindano hayo 
Meneja wa Mkwabi Super Market ambao ndiyo wadhamini wa Mashindano hayo,Lawi Sozigwa 

***
ZAIDI ya magari 12 yanatarajiwa  kushiriki kwenye michuano ya Mbio za Magari ya Mkwabi Tanga Rally 2018  yatakayoanza leo Jumamosi na Jumapili kwenye eneo la Super Market ya 
Mkwabi Jijini Tanga kuzunguka maeneo mbalimbali mkoani hapa na kurejea  yalipoanzia.

Hayo yalibainishwa leo na Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari Mkoani  Tanga (TMSC) Akida Machai wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu kuelekea mashindano hayo.

Alisema maandalizi ya mashindano hayo hivi sasa yanaendelea vizuri  ikiwemo kufanya mazungumzo na Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama  Barabarani,Jeshi la Zimamoto na Madaktari kwenye hospitali ya mkoa wa  Tanga Bombo.

“Kwa kweli haya ndio mashindano ya kwanza tokea mwaka huu ulipoanza  hivyo tutahakikisha yanafanyika kwa mafanikio makubwa kwa lengo la kutoa burudani kwa wakazi wa maeneo yatakapokuwa yakipita kama ilivyokuwa  miaka ya nyuma ",alisema.

Kwa upande wake,Mratibu wa Mashindano ya Magari Tanzania,Faheem Alo  alisema msimu huu mashindano hayo yatakuwa ya aina yake kutokana na  kufanya maandalizi mapema jambo ambalo limeongeza hamasa.

Alisema mashindano hayo yataanza saa mbili asubuhi eneo la Mkwabi Super  Market kuelekea eneo la Pongwe km 15 toka Tanga mjini na baadae kuelekea kwenye maeneo waliopangiwa kwa ajili ya kupita hivyo kuwataka wakazi wa Jiji hilo kuona namna ya kujitokeza kwa wingi kuweza kushuhudia namna 
madereva wanavyochuana.

Aidha alisema kwa siku ya Jumapili mashindano hayo yataanzia Hotel ya  Tanga Beach kuelekea Mkinga na baadae kwenda Duga Sigaya ambapo kwenye  maeneo ambayo yatapita wananchi wametakiwa kuwa makini na watoto wao.

“Tumejipanga vizuri kwenye masuala ya ulinzi na usalama kwa kuzungumza  na askari wa usalama barabarani wakiwemo wa Jeshi la Zimamoto kwa  lengo la kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mashindano hayo".alisema.

Hata hivyo aliwataka watu kuhakikisha wanazuia familia zao
zisijitokeze barabarani wakati mashindano hayo yanaendelea kwa lengo la kuepukana na madhara wanayoweza kukumbana nayo.

Naye kwa upande wake,Meneja wa Mkwabi Super Market ambao ndio wadhamini  wa Mashindano hayo,Lawi Sozigwa alisema kampuni hiyo imelenga  kuhakikisha mchezo huo unapata mafanikio makubwa na ndio maana wakaona  watoe mchango wao huo.

Alisema pia watatumia mashindano hayo kuweza kujitangaza kwa jamii ya  wakazi wa mkoa wa Tanga na nje ya mkoa kwa lengo la kuweza kutambulika  zaidi.

“Sisi kama Mkwabi Super Market tumekuwa wafadhili wa mashindano hayo na  sasa ni mwaka wa pili huu hivyo nisema tu tunatumia nafasi hii pia  kuweza kujitangaza",alisema Sozigwa.

(Habari kwa hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527