BRELA YATOA MIEZI SITA WAMILIKI WA KAMPUNI KUHAKIKI TAARIFA ZAO MTANDAONI

Ili kuhakikisha huduma zote zinatolewa kidigitali, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) umetoa miezi sita kwa wamiliki wa kampuni kuhakiki taarifa zao kwenye mfumo mpya kwa njia ya mtandao, vinginevyo hawatapata huduma wanazostahili.


Agizo hilo linazihusu kampuni 200,000 zilizosajiliwa kabla ya Februari mosi mwaka huu baada ya mfumo huo kuanza kutumika Januari 4.


Ofisa mtendaji mkuu wa Brela, Frank Kanyusi alisema mpaka sasa ni kampuni 200 pekee zimesajiliwa kwenye mfumo huo na kufafanua kuwa, hakuna kampuni itaweza kufanya lolote kwani mifumo yote ya Serikali inaangalia ripoti ya Brela kabla ya kumhudumia mteja.


“Kama hujahakiki taarifa na kuingia kwenye mfumo wa mtandao, hakuna chochote unachoweza kufanya kwa kuwa hata mamlaka nyingine kama (Mamlaka ya Mapato Tanzania) TRA lazima zije kwetu kujiridhisha kuhusu kampuni fulani. Hivyo, iwapo haijasajiliwa haitapata huduma,” alisema.


Kwenye mfumo huo, mmiliki wa kampuni anaweza kufanya mabadiliko yoyote kwa njia ya mtandao, hivyo kupunguza gharama ya kusafiri kutoka mikoani mpaka Dar es Salaam zilipo ofisi za wakala huo.


“Sasa hivi chochote kinafanyika mtandaoni, tukijiridhisha tunaingiza kwenye nyaraka zetu kama hatujaridhika tunawasiliana na mhusika,” alisema Kanyusi.


Alisema kinachotakiwa kampuni kujisajili kwenye mfumo huo ni namba ya ulipajikodi, namba ya mlipakodi ya kila mkurugenzi, vitambulisho vya uraia vya wakurugenzi na wenye hisa ndani ya kampuni.


Tangu mfumo huo uanze kufanya kazi, Kanyusi alisema umerahisisha utoaji huduma. “Tumeshaanza kupata mrejesho kutoka kwa mawakala wa alama za biashara, wanasema umewaondolea usumbufu na umewarahisishia utendaji wao tofauti na ilivyokuwa awali wakati kazi zilipokuwa zikifanyika kwenye karatasi,” alisema.


Muda wowote kuanzia sasa, Brela inatarajia kuzindua utoaji leseni daraja A na B kwa njia ya mtandao, huku ikiwa imejiwekea malengo ya kusajili zaidi ya kampuni 50 kwa siku kupitia mfumo huo.


Kanyusi alisema Brela ndiyo mlango wa kurasimisha biashara hivyo inaweka mazingira rahisi ya kuanzisha biashara na kuvutia wawekezaji.


“Tunafahamu zitakuwapo changamoto za hapa na pale kwenye mfumo huu mpya ila ninaamini tutafika, wenye kampuni wazivumilie watakazokumbana nazo ila wasajili kampuni zao,” alisema.


Mfumo huo unaotumiwa na Brela unaziunganisha mtandaoni taasisi muhimu za Serikali zinazohusika na usimamizi wa biashara, ili kuokoa muda kwa wahusika kuzifuata kwenye ofisi zilizopo maeneo tofauti.


Kanyusi alisema faida nyingine za mfumo huo ni kupunguza gharama na muda wa kusajili na kuanzisha biashara nchini. Kabla ya kuanza kuutumia mfumo huo, Brela ilienda kujifunza kwenye mataifa mbalimbali kuhusu ufanisi wake ikiwamo Vietnam unakotumika kwa miaka mingi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527