AFISA WA TRA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA RUSHWA

Ofisa Msaidizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Joyce Amon amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala akikabiliwa na shtaka la kushawishi rushwa.


Wakili wa Serikali, Sophia Nyanda alisema jana Ijumaa Machi 9, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Adelf Sachore kuwa Desemba 12, 2017 katika eneo la Gerezani Kariakoo Wilaya ya Ilala mshtakiwa huyo akiwa mwajiriwa wa TRA kama Ofisa Msaidizi wa Kodi alishawishi rushwa ya Sh800,000 kutoka kwa Antelo Sanga ili asiweze kumwandikia cheti cha faini cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).


Katika shtaka la pili, mwanafunzi Lilian Wilson (23) naye anakabiliwa na shtaka la kusaidia kutenda kosa hilo.


Wakili Nyanda alidai Desemba 13,2017 katika Hoteli ya Tansome mshtakiwa huyo Lilian alimsaidia Joyce ambaye ni Ofisa Msaidizi wa Kodi wa TRA kujipatia Sh400,000 kutoka kwa Antelo Sanga ili asiweze kumpatia cheti cha faini cha VAT.


Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.


Hakimu Sachore alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua kutoka katika taasisi zinazotambulika kisheria ambao watasaini ahadi ya Sh5 milioni kwa kila mmoja. Na kwamba barua hizo zitahakikiwa.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 20, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527