Monday, February 12, 2018

SHULE ZA MKIANI ZAMKERA RAIS

  Malunde       Monday, February 12, 2018

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesikitishwa na shule saba za Zanzibar kuwa mkiani katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka jana, na kuuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali uandae mkutano maalumu na walimu wa shule hizo saba zilizofanya vibaya kwa Tanzania nzima.

Dk Shein aliyasema hayo jana katika Ukumbi wa Baraza la Zamani la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Unguja katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Sitawa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU).

Licha ya kuipongeza wizara hiyo na walimu wote kwa matokeo mazuri yaliyopatikana kwa niaba yake na serikali kwa jumla kutokana na ufaulu wa wanafunzi wote waliofanya mitihani ya Taifa wakiwemo wa darasa la nne, darasa la sita, Kidato cha Pili, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita, ameonesha masikitiko kwa Kidato cha Nne.

 Hali hiyo imetokana na ufaulu wa kidato cha nne kushuka, na hivyo shule saba za sekondari za Zanzibar zimo katika orodha ya shule 10 zilizofanya vibaya kwa Tanzania nzima mwaka 2017.

Alieleza kuwa katika mkutano huo wajadili sababu zilizosababisha shule hizo zifanye vibaya sambamba na kuandaa mkakati maalumu ili kuondokana na tatizo hilo na kumtakawaziri husika kuongoza mkutano huo. 

Alisikitishwa na hali hiyo na kueleza kuwa wanafunzi wa Zanzibar wanaweza kufanya vizuri iwapo watapata maelekezo mazuri kutoka kwa walimu wao kwani Zanzibar ina historia nzuri kielimu.

Dk Shein alisema serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya elimu kila mwaka, ili sekta hiyo izidi kuimarika, ambako Sh bilioni 120.726 ziliingizwa katika wizara hiyo mwaka 2015/16, Sh bilioni 133.501 mwaka 2016/17 na Sh bilioni 197.290 mwaka 2017/18 na kuahidi kuongeza zaidi kwa mwaka 2018/2019.

Alieleza kuwa wapo baadhi ya walimu wanaoharibu fani ya ualimu ambayo ni yenye heshima kubwa kutokana na tamaa zao na wale wanaoingiza siasa katika fani hiyo huku akieleza kukerwa na tabia ya baadhi ya walimu kufanya biashara ya urojo na biskuti shuleni huku wakisingizia kushuka kwa elimu wakati wao ndiyo chanzo. 

Aidha, Dk Shein alieleza kuwa katika kuongeza ufanisi wa maendeleo ya shule, suala la ukaguzi wa shule na walimu ni muhimu, lakini kwa bahati mbaya suala hilo limekuwa halifanywi vizuri.

Pia, alieleza kuwa wakati alipofanya ziara za mikoa Agosti 2017 aliagiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ushirikiane na viongozi wa mikoa na wilaya katika kuzifanyia kazi changamoto za kuwepo kwa utoro uliokithiri wa walimu na wanafunzi, lakini hadi leo hajapelekewa taarifa yoyote.

Kaimu Waziri wa wizara hiyo, Mahamoud Thabit Kombo ambaye pia ni Waziri wa Afya alieleza kuwa miongoni mwa sababu zinazofanya kuwepo kwa changamoto katika elimu ikiwamo wingi wa wanafunzi madarasani ni kuongezeka kwa idadi ya watu Zanzibar hasa ikizingatiwa kuwa katika nchi za Afrika, idadi ya watu Zanzibar imekuwa ikiongezeka kwa asilimia kubwa. 

Naye Rais wa chama hicho, Mwalimu Seif Mohamed alitoa pongezi zake kwa Rais Shein kutokana na juhudi za makusudi anazozichukua katika kuangalia maslahi ya wafanyakazi wa serikali wakiwemo walimu.
Chanzo- Habarileo
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post