Picha : DC SHINYANGA AFANYA OPARESHENI YA USAFI NA MAZINGIRA,AKAMATA NA KUTOZA FAINI WENYE MITI ILIYOKUFAMkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ameendesha oparesheni ya usafi na Mazingira kukagua usafi na miti iliyotelekezwa na kuwawajibisha wananchi ambao miti yao imekufa kwa kulipa faini ya shilingi 50,000/= kwa kila mti na kuwataka wapande miti mingine.

Mkuu huyo wa wilaya amefanya oparesheni hiyo Februari 24,2018 katika mitaa mbalimbali mjini Shinyanga ambapo kila mwananchi ambaye miti iliyopandwa kwenye eneo lake imekufa aliwajibishwa kwa kufanya uzembe na kusababisha miti ife.

Katika opareshini hiyo kila mwananchi aliyepigwa faini alikuwa anapatiwa risiti ya malipo na aliyeshindwa kulipa alikuwa anapandishwa kwenye gari la polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

Akizungumza wakati wa oparesheni hiyo Matiro ambaye alikuwa ameambatana na maafisa mbalimbali na askari polisi alisema hataki kuona miti iliyopandwa kupitia kampeni ya upandaji miti iliyozinduliwa Septemba 23,2017 yenye kauli mbiu ya ‘Shinyanga Mpya,Mti Kwanza’ inakufa kwa uzembe kwani walikubaliana kila mwananchi atunze miti hiyo.

“Miezi mitano iliyopita tulianzisha kampeni ya upandaji miti wilayani hapa ili kuboresha mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha jangwa,tukapanda miti na kumtaka kila mwananchi atunze iliyopo kwenye eneo lake”,alieleza Matiro.

“Nimeanza kukagua miti hii ili nione imefikia hatua gani,kama mti uliopo kwenye eneo lako lazima tukuwajibishe,wote tuliokuta miti imekauka tumewapiga faini ya shilingi 50,000/=”,aliongeza.

Matiro alisema wilaya hiyo imepiga marufuku kwa mifugo kuzurura mitaani,ikikamatwa kwa kila mfugo faini ni kati ya shilingi 50,000/= na 100,000/=,iwe ng’ombe,mbuzi,kondoo au punda, tukikuta mti umekauka faini ni shilingi 50,000/=.

Afisa Misitu wa Manispaa ya Shinyanga,Emmanuel Nyamwihura alisema wanatoza faini hizo kwa mujibu wa sheria ya Usafi na Mazingira ya Mwaka 2014.

ANGALIA PICHA WAKATI WA OPARESHENI HIYO
Mmoja wa wananchi katika kata ya Ibinzamata akijitetea kwa kuonesha dumu la maji alilokuwa analitumia kumwagilia maji mti wake uliokufa.Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro. Kushoto ni Afisa Misitu wa Manispaa ya Shinyanga,Emmanuel Nyamwihura - Picha zote na Kadama Malunde1 blog
Wananchi ambao miti iliyopandwa mbele ya makazi au biashara zao imekufa wakipanda kwenye gari la polisi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akimpongeza mwananchi ambaye miti yake imekua vizuri.
Mwananchi akionesha mti wake uliokufa kabla ya kulipa faini ya shilingi 50,000/=.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwahoji wananchi ambao miti yao imekufa.
Maafisa walioambatana na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro wakizungumza na mmiliki wa Nyumba ya Kulala wageni ya Masanja Safari Logde ambaye miti iliyokuwa imepandwa mbele ya nyumba hiyo imekufa.
Kulia ni Mwananchi akitetea kwanini miti aliyopanda imekufa.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwataka wafanyabiashara waliopo karibu na Benki ya NMB Manonga kupanda miti katika eneo lao la biashara.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiangalia sehemu ambayo imepandwa mawe badala ya mti katika eneo la Mnara wa Voda mjini Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiipongeza ofisi ya CCM wilaya ya Shinyanga Mjini kwa kukuza miti vizuri mbele ya ofisi hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiangalia mwananchi anavyotoa vijiti vilivyowekwa kwenye mti ambao tayari umestawi vizuri.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiangalia jinsi waendesha bodaboda katika eneo la Kambarage wanavyoondoa maganda ya miwa yaliyotapakaa katika eneo hilo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitoa maagizo kwa mama lishe katika eneo la Kambarage kuondoa uchafu na kuzuia maji machafu katika eneo lake la biashara.
Wananchi ambao miti yao imekufa wakiwa katika gari la polisi.
Katikati ni Afisa Misitu wa Manispaa ya Shinyanga,Emmanuel Nyamwihura akiangalia Nyanya iliyopandwa badala ya mti.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwataka wananchi waliokamatwa kuhakikisha wanapanda miti kwenye maeneo yao.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post