MWANAUME ACHOMOKA KWENYE BOTI NA KUJIRUSHA BAHARINI KINA KIREFU SAFARI YA ZANZIBAR

Mwanaume mmoja ambaye jina lake bado halijafahamika amejirusha baharini kutoka katika boti ya Azam iliyokuwa ikitokea jijini Dar es Salaam kuelekea Zanzibar Jumatatu, katika eneo linalohisiwa kuwa na kina kirefu.



Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii jana inaonyesha boti hiyo ikiwa imesimama eneo ambalo mwanaume huyo alijirusha huku watu wakijadiliana namna ya kumwokoa.


Tukio hilo limeelezwa kufanyika katika eneo la Bahari ya Hindi "ukishapita Msasani" ambako kuna mkondo wa maji unaodhaniwa kusababishwa na kina kirefu cha maji.


Eneo hilo lipo mwendo wa nusu saa kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kwa boti ziendazo kasi. Safari mpaka Zanzibar huchukua saa mbili.


Video hiyo inaonyesha abiria hao wakiwa wanashangaa uamuzi wa mtu huyo kujitosa baharini huku wengine wakisikika wakisema kuwa anaonekana akiogelea.


Baadhi ya waliokuwa kwenye boti hiyo walisikika kwenye video hiyo wakiomba wapewe nafasi wajitose kwenda kumtafuta kwani wao ni mahiri kwenye uogeleaji.


"Kama vipi tumfuate, wengine tunaweza (kuogelea)... anaonekana yule, kuleee tuacheni sisi tunaoweza kuogelea tukamchukue kwasababu tunaweza jamani," alisikika mtu huyo akimwomba mmoja wa wahudumu wa boti hiyo huku akirekodi video.


Taarifa kutoka ndani ya Azam zilisema mabaharia wa boti hiyo walijitahidi kumtafuta mwanaume huyo eneo alipojitosa lakini hawakufanikiwa.


"Baada ya mwanaume huyo kujirusha baharini nahodha wa boti aliambiwa na aliirudisha boti nyuma hadi eneo linalodhaniwa kuwa ndipo alipojitosa, lakini hawakufanikiwa (kumuona). Walirudi wenyewe tu," alisema mmoja wa mashuhuda.


Aidha, shuhuda huyo alisema baada ya kumkosa, walijadiliana kwa muda kuhusu nini kinaweza kufanyika na hatimaye waliona hawana namna zaidi ya kuendelea na safari ya Zanzibar.


Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo alisema waulizwe watu wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.


Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema ofisi yake bado haijapewa taarifa yoyote kuhusu mkasa huo.


"Sasa kama amejitosa baharini wanasema amekufa au wamefanikiwa kumwokoa?" Aliuliza Kamanda Mambosasa. "Mimi hizo taarifa ndiyo kwanza nazisikia kutoka kwako."


Aprili 5, mwaka jana msichana mmoja mwenye umri wa miaka 16 aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika sekondari moja ya Zanzibar, alijitosa baharini katika eneo la Chumbe.


Msichana huyo alijirusha kutoka katika boti ya Azam ya Kilimanjaro V akisafiri na mjomba wake kutoka jijini kuelekea Unguja, lakini aliokolewa na mabaharia wa chombo hicho.


Baadaye wanafamilia wa msichana huyo waishio Kikwajuni, Unguja walisema chanzo cha msichana huyo kutaka kujiua ni kukutwa na simu ambayo alishindwa kueleza alikoipata na kukimbilia Dar es Salaam kabla ya kufuatwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527