MRADI WA “UZAZI UZIMA” KUIMARISHA ZAIDI HUDUMA ZA AFYA YA UZAZI MKOANI SIMIYU



Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Health Afrika nchini Tanzania Dkt.Florence Temu (katikati) na kulia ni Mkuu wa Miradi shirika la Amref Dkt.Aisa Muya. Mazungumzo hayo yalifanyika Bariadi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa shirika la Amref Dkt.Florence Temu, Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Antony Mtaka.Awali Mkurugenzi Mkazi wa shirika la Amref akitoa salamu zake mbele ya Makamu wa Rais.Meneja Mradi wa Uzazi na Uzima kutoka shirika la Amref, Elia Msegu akizungumza na wanahabari.

Na BMG

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Health Afrika nchini Tanzania Dkt.Florence Temu, amesema utekelezaji wa mradi wa Uzazi Uzima mkoani Simiyu, utasaidia kuboresha zaidi huduma za afya ya uzazi mkoani humo na hivyo kupunguza tatizo la vifo kwa akina mama na watoto wakati wa kujifungua.

Dkt. Temu alitoa kauli hiyo juzi Februari 21,2018 baada ya kukutana na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa na ziara ya kikazi mkoani Simiyu na kumweleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo mkoani humo.

Alisema mradi huo ambao unatekelezwa katika halmashauri za Bariadi Vijijini, Bariadi Mjini, Busega, Itilima, Meatu na Maswa utahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa huduma za afya katika Zahanati, Vituo vya Afya pamoja na hospitali kwa kufanya ukarabati, kutoa vifaa tiba pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma za afya.

Meneja Mradi huo wa Uzazi Uzima kutoka shirika la Amref, Elia Msegu alisema pia utawajengea uwezo wananchi na wadau wengine wakiwemo viongozi wa dini na kimila ili kutambua umuhimu wa akina mama kujifungulia katika vituo vya afya badala ya nyumbani.

Uzazi Uzima ni mradi wa miaka minne ambao ulianza tangu mwaka jana mkoani Simiyu na utafikia tamati mwaka 2020 ukifadhiliwa na serikali ya Canada kupitia kitengo cha Global Affairs Canada (GAC) na kutekelezwa na mashirika ya Amref, Marie Stopes pamoja na Deloitte ambapo unatarajiwa kuwanufaisha moja kwa moja zaidi ya wananchi laki sita pamoja na wanufaika wasio wa moja kwa moja zaidi ya milioni moja, ukigharimu zaidi ya shilingi bilioni 18 za kitanzania.



Bonyeza HAPA kusoma zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527