MHANDISI AVULIWA MADARAKA KWA KUMLIPA MAMILIONI YA FEDHA MKANDARASI MRADI HEWA WA MAJI


NAIBU Waziri wa Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda amemvua madaraka Mhandisi wa Maji wilayani Chemba, mkoani Dodoma, Rodrick Mbepera kwa kushindwa kusimamia mradi ya maji na kumlipa mkandarasi mradi ambao hautoi maji.

Aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Lahoda mara baada ya kutembelea mradi wa Maji wa Kijiji cha Lahoda/Kisande katika Kata ya Lahoda, wilayani Chemba. Kakunda alisema alibaini kuwa katika mradi huo mkandarasi amelipwa fedha nyingi za ukarabati ambao umefanyika chini ya kiwango, haujakamilika na hautoi maji na huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa adha ya kukosa maji.

“Sijaridhishwa na ukarabati wa mradi huu, umefanyika chini ya kiwango, usanifu wake si wa kitaalumu na matangi yamejengwa chini ya kiwango, tayari yamepasuka hata kabla hajayaanza kujazwa maji,” alisema Naibu Waziri Kakunda kwa masikitiko. Mhandisi Mbepera alipohojiwa na Naibu Waziri, alikiri kwamba mradi huo wa maji uliokarabatiwa na mkandarasi ‘Mrimi International Tanzania Limited’ ulipangwa kukamilika Oktoba 2014, haujakamilika hadi sasa na tayari mkandarasi huyo alikwishalipwa zaidi ya Sh milioni 367.6 kati ya Sh milioni 451.4 zilizotolewa na serikali lakini pia mradi hauotoi maji.

Naibu Waziri alimvua madaraka kutokana na kitendo cha kumlipa mkandarasi huyo kiwango cha fedha kikubwa wakati ukarabati umefanyika chini ya kiwango na mradi hautoi maji na kushushwa cheo hicho. Kwa hatua hiyo Mhandisi huyo anapoteza haki zake alizokuwa akipata kwa kusimamia Idara ya Maji pamoja kukosa fedha za mawasiliano, nyumba na usafiri na fedha nyingine zinazofikia Sh milioni 1.

Naibu Waziri Kakunda alimshangaa mkandarasi huyo badala ya kuanza kukarabati kisima kwa kufukua na kuweka pampu ili kusukuma maji na kubaini kiwango cha maji kilichopo ndani, mkandarasi alianza kujenga na kukarabati matangi, baadaye akabaini kwamba kiwango cha maji kimepungua kutoka lita 12,950 hadi lita 2,400.

Halmashauri ya Chemba baada ya kushituka kwamba mkandarasi huyo hajatekeleza kazi nyingi za mradi huo na tayari fedha nyingi amelipwa, iliamua kushikilia jumla ya Sh milioni 83.7 zikiwemo Sh milioni 40.84 za amana ya kufanya kazi hiyo na Sh milioni 42.92 ambazo zilizuiliwa kutokana na mkandarasi huyo kutokamilisha kazi ya mradi huo ambao hautoi maji. Wakati akikagua mradi huo, Naibu Waziri alisikitishwa na kiwango cha fedha ambacho amekishalipwa cha Sh milioni 367.6 wakati kisima hakijafukuliwa na matangi yamekarabatiwa chini ya kiwango na mbaya zaidi mradi hautoi maji.

Ili kuukwamua mradi huo, Kakunda alimwagiza Mhandisi Mbepera kupeleka wizarani Mkataba wa mradi huo kati ya halmashauri na mkandarasi, nyaraka zinazoonesha jumla ya gharama za ujenzi na ukarabati na akamtaka Mkaguzi wa Ndani apeleke karatasi ya fedha za benki kuhusu mradi huo. Pia alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Dk Semistatus Mashimba kumtafuta mtu mwingine kukaimu nafasi ya Mhandisi wa Maji, lakini pia alimtaka kwenda kuwaandikia barua Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) ili kuchunguza kisima hicho kama kinaweza kufukuliwa na kuweka pampu ya kuvuta maji kutoka ardhini.

Alisema DDCA wakikagua mradi huo, ikiwezekana wapewe kazi ya kuchimbua kisima hicho, kwa kutumia Sh milioni 83.7 zinazoshikiliwa na halmashauri ili kuhakikisha wananchi takribani 9,000 wa vijiji viwili hivyo wanapata maji mapema.

Pia alimwagiza Mhandisi wa Maji Mkoa, Athuman Mathayo kwenda kuweka kambi kwenye mradi huo kijijini hapo Lahoda ili kuhakikisha ukarabati wa mradi unafanyika na unakamilika ili kuwaondolewa adha wananchi ya kukosa maji kwa muda mrefu.

Mbunge wa Jimbo la Chemba, Juma Nkamia CCM), alimwomba Naibu Waziri wa Maji kuwaondoa watendaji wa Idara ya Maji ambao wanakwamisha miradi ya maji wilayani humo ikiwezekana Tamisemi iunde Kamati Maalumu kuchunguza miradi ya maji ambayo mingi imevurugwa na haitoi maji. Naibu Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma (Maji), Mathayo alisema uongozi wa mkoa ulitoa ushauri kwa mhandisi huyo wa kuangalia uwezekano wa kufukua kisima hicho ili kujua kiwango cha maji, lakini ushauri huo haukuzingatiwa na hadi leo maji hayatoki kwa wananchi.

Akizungumza Mhandisi wa Maji kutoka Ofisi ya Rais- Tamisemi, Kilanga Maganya alisema pamoja na mhandisi huyo kushindwa kusimamia mradi wa ukarabati bado hajaonesha kujiamini katika utendaji wa kazi zake.

Kaimu Mtendaji wa Kata ya Luhoda, Juma Ibuva alisema, mradi huo ungekamilika ungewasaidia kupata maji jumla ya wananchi 9,084 wakiwamo wananchi 7,620 wa Lakoda na wananchi 1,464 wa Kisuda ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikosa huduma ya maji. Mradi huo ulianza kujenga tangu mwaka 1969 na hadi mwaka 1973 ulishindwa kufanya kazi, na ndipo Wilaya ya Chemba, Julai 15, 2014 ilisaini mkataba wa ukarabati wa miundombinu ya maji na mkandarasi ‘Mrimi Intenational (T) Limited’ ambaye alishindwa kuukamilisha.

IMEANDIKWA NA MAGNUS MAHENGE - HABARILEO DODOMA
Theme images by rion819. Powered by Blogger.