CHADEMA WASITISHA KAMPENI ZA UDIWANI MULEBA


Viongozi wa Chadema wilayani Muleba Mkoa wa Kagera, wamesitisha shughuli za kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa Buhangaza Mchungaji Nelson Athanasio Makoti ili kupata nafasi ya kushughulikia matibabu yake baada ya kuhamishwa Hospitali ya Kagondo hadi Dar es Salaam kwa matibabu.


Katibu mwenezi wa Chadema Muleba Kusini, Hamisi Yusufu amesema hawezi kutaja alikolazwa mgombea huyo kwa sababu za kiusalama kutokana na hali ya upepo ulivyo kisiasa hapa nchini.

Amesema kampeni za uchaguzi wa udiwani Kata ya Buhangaza, zitaendelea kesho.

"Suala la wapi mgombea amelazwa msemaji wake anaweza kuulizwa Tumaini Makene lakini kwa taarifa nilizopokea asubuhi ya leo ameonyesha mabadiliko tofauti na ilivyokuwa Kagondo," amesema Yusufu.

Hata hivyo, amesema wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu na kwa sasa Chadema hawaelekezi tuhuma zozote kwa kundi lolote la kisiasa.

Amesema jukumu kubwa ni vyombo vya dola kufanya kazi ya kuchunguza na kubaini waliohusika kwa kusababisha mgombea kuathirika kiafya.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Isack Msangi amesema katika mahojiano na Makoti na ndugu zake na wananchi hakuna mtuhumiwa anayeshikiliwa japo upelelezi unaendelea.

Msangi amesema saa tisa alasiri ya leo jeshi hilo litatoa ufafanuzi kuhusu mwenendo wa kufuatilia tukio la mgombea huyo na mahali alipo ili kuwaweka sawa wananchi wanaofuatilia kinachofanyika dhidi ya mpendwa wao.


Na Shaaban Ndyamukama ,Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527