RAIS MAGUFULI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO ZA MABALOZI 6 WALIOTEULIWA KUZIWAKILISHA NCHI ZAO TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Januari, 2018 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 6 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.


Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni Balozi wa Nigeria hapa nchini Mhe. Sahabu Isah Gada, Balozi wa Poland hapa nchini Mhe. Krzysztof Buzalski, Balozi wa Uturuki hapa nchini Mhe. Ali Davutoglu, Balozi wa Ufaransa hapa nchini Mhe. Frédéric Clavier, Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Noah Gal Gendler na Balozi wa Australia hapa nchini Mhe. Alison Chartres.


Akizungumza na Mabalozi hao Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na ameahidi kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na nchi hizo.


Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kutilia mkazo ushirikiano katika masuala ya kiuchumi yakiwemo kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo kuja kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini, hususani katika viwanda, kilimo, utalii na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kwamba Serikali itakuwa tayari wakati wote kujenga mazingira bora ya kufanikisha biashara na uwekezaji huo.


Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kufikisha salamu zake kwa viongozi wa nchi zao, na kuwakaribisha kuitembelea Tanzania ili kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Januari, 2018

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527