RAIS MAGUFULI AMTUMIA SALAMU ZA RAMBIRAMBI RAIS WA KENYA KUFUATIA AJALI YA BARABARANI ILIYOUA WATU 34

"Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa ajali iliyosababisha ndugu zetu takribani 36 kupoteza maisha baada ya basi la abiria kugongana na roli katika barabara ya Nakuru - Eldoret nchini Kenya.
 
Msiba huu umesababisha majonzi makubwa sio tu kwa ndugu zetu wa Kenya bali pia kwetu sote wana Jumuiya ya Afrika Mashariki, tumepoteza wapendwa wetu na nguvu kazi yetu.
 
Kwa niaba ya Watanzania wote nakupa pole sana ndugu yangu Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya kwa msiba huu mkubwa ulioupata, nawapa pole wana familia wote waliowapoteza jamaa zao na pia nawapa pole wananchi wote wa Kenya.
 
Naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, nawaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka na Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina".
 
Hizi ni salamu za rambirambi alizozitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kufuatia ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya watu takribani 36 baada ya basi la abiria kugongana na roli katika barabara ya Nakuru - Eldoret nchini humo tarehe 31 Desemba, 2017.
 
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Desemba, 2017

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527