RAIS MAGUFULI AKATA MZIZI WA FITINA KUONGEZEWA KIPINDI CHA URAIS

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 13 Januari, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole, Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Baada ya mazungumzo hayo Ndg. Polepole amesema Mhe. Dkt. Magufuli amemuelekeza kuwajulisha wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala unaoendelea juu kuongezwa kwa kipindi cha Urais kutoka miaka 5 iliyowekwa kwa mujibu wa katiba, hadi miaka 7.


Ndg. Polepole amesema Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kwa ujumla kuupuuza mjadala huo kwa kuwa haujawahi kujadiliwa katika kikao chochote cha chama, na ni kinyume na katiba ya CCM na katiba ya nchi.


Ameongeza kuwa Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wana CCM na umma wa Watanzania kutokubali kuyumbishwa ama kupotoshwa na mambo yasiyokuwa ya msingi na badala yake wajielekeze katika ajenda muhimu ya kujenga uchumi na kutekeleza Ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.


Ndg. Polepole amebainisha kuwa Mhe. Dkt. Magufuli hana mpango wowote na hatarajii kuongeza kipindi cha Urais wakati wote wa uongozi wake.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Januari, 2018

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527