ALIYEJIUNGANISHIA BOMBA LA MAFUTA NYUMBANI KWAKE NI MSTAAFU WA TAZAMA


Aliyejiunganishia bomba la mafuta nyumbani kwake Samwel Kilanglani(63) amejulikana kuwa ni mfanyakazi mstaafu wa bomba la kusafirisha mafuta Tanzania na Zambi (TAZAMA).


Kilanglani anatuhumiwa kutoboa bomba la mafuta ya dizeli la Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) na kujiunganishia kwenye mantaki mawili yakiwa ndani ya nyumba yake iliyopo Tungi Kigamboni.

Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika amesema mtuhumiwa huyo alijiunganishia na bomba la TPA kwa njia ya kuchomelea na kuunganisha moja kwa moja kwenye mantaki yake mawili yaliyochimbiwa chini ndani ya nyumba yake.

Kitalika amesema mtuhumiwa alijiunganishia katikati na bomba kuu hivyo mafuta yanapopelekwa sehemu husika mengine yanaingia kwake hivyo hayafiki kama yalivyokusudiwa.


"Mafuta yanaweza yakapelekwa lita 4,000 sehemu husika lakini hayafiki yote mengine yanaenda kwa mtuhumiwa huyu matokeo yake wanajiuliza haya mengine yameenda wapi," amesema.

Kamanda wa Kikosi cha Polisi Bandari, Robert Mayalla amesema inavyoonekana huyu mtuhumiwa alijiunganishia kipindi mabomba hayo yanajengwa kwa kuwa kipindi hiki isingewezekana.

Amesema bomba hilo amejiunganisha kwa utaalamu wa juu kwa kuwa hayo mabomba yamepitishwa chini ya ardhi.

Wakati hao wakisema hivyo Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko amesema anaandaa ripoti kuhusu tukio hilo na ataitoa saa tisa leo Jumanne.



"Hili ni suala kubwa linalohusu uchumi wa nchi. Ni sawa na mtu kuvamia kambi ya jeshi."







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527