ZITTO KABWE : WAPINZANI WALIOHAMIA CCM HAWAMUUNGI MKONO JPM BALI WAPO KWA AJILI YA MADARAKA NA AHADI WALIZOPEWA

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe amesema wanachama wa Chama hicho waliohamia Chama cha Mapinduzi (CCM) sio kweli wanaunga mkono juhudi za Rais bali ni kwa ajili ya madaraka na ahadi walizopewa.


Hayo ameyasema jana kwenye hotuba yake kwa Kamati Kuu Juu ya chama hicho juu ya Hali ya Siasa Nchini Tanzania. 


Mh. Zitto alieleza kuwa hoja inayotolewa na wanachama wanaohama ACT Wazalendo ya kuunga mkono jitihada za Rais haina mashiko kwani walikuwa na nafasi ya kuunga mkono wakiwa ndani ya chama hicho.


"Takribani watu wote wanaoondoka kutoka vyama vya upinzani kwenda chama tawala wanasema wanaunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa Chama Tawala katika uendeshaji wa nchi yetu. Hii sababu haitoshi kueleza maamuzi yao, hususani kwa wale wanaotoka chama chetu cha ACT Wazalendo", alisema Zitto.


Kiongozi huyo wa Chama aliongeza kuwa Halmashauri Kuu ya Chama iliyooketi katika ukumbi wa Jeshi la Wokovu, Aprili, 2016 iliazimia masuala ambayo chama hicho kinaweza kuunga mkono ikiwemo mapamabno dhidi ya Ufisadi.


"Ni dhahiri kuwa wenzetu wana sababu zaidi ya kumuunga mkono Rais, kuna ambao sababu ni vyeo walivyopewa, na wengine ahadi za vyeo watakavyopewa", alisema Zitto.


Chama Cha ACT Wazalendo hivi karibuni kimeondokewa na wanachama wake waandamizi ambao ni Profesa Kitila Mkumbo, Anna Mghwira, Albert Msando, Samson Mwigamba na Edna Sunga. Wote wamejiunga na CCM.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527