WAZIRI MKUU NAYE AWASILISHA TAMKO LA MALI NA MADENI YAKE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema amekwishawasilisha tamko la maadili ya viongozi wa umma kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma tangu Alhamisi Desemba 28, 2017.


Akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake Namahema ‘A’ wilayani Ruangwa mkoani Lindi jana jioni (Ijumaa, Desemba 29, 2017), Waziri Mkuu alisema fomu hizo zilipokelewa na amekwishapatiwa barua ya kupokea tamko hilo.


“Nimewaita hapa ili kuthibitisha kuwa nimetekeleza takwa hilo la kisheria na tayari Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ya Umma imekiri kupokea tamko langu kwa barua hii hapa,” alisema Waziri Mkuu huku akionyesha barua hiyo ambayo ilisainiwa na Jaji Harold Nsekela, Desemba 28, 2017.


“Kwa kuzingatia mfano ulioonyesha na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ninawaagiza viongozi wote wanaotakiwa kujaza fomu hizo kwa mujibu wa sheria wafanye hivyo na kuziwasilisha ifikapo tarehe 31 Desemba, 2017 saa 10 jioni,” alisisitiza Waziri Mkuu.


Alisema anawakumbusha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu wote na viongozi wote walioko kwenye ngazi za uteuzi wahakikishe wanatimiza takwa ambalo liko kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya Mwaka 1995.


Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwatakia Watanzania wote heri wakati wanaposubiri kumaliza mwaka 2017 na kuwatakia heri na fanaka katika maeneo waliyopo wanapojiandaa kuupokea mwaka 2018.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527