VYAMA SITA VYA UPINZANI VYASUSIA UCHAGUZI TANZANIA....WADAI CCM,SERIKALI WANATUMIA MABAVU




Siku 26 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo matatu nchini, vyama sita vya upinzani vimesema havitashiriki kutokana na mazingira ya ushindani kutokuwa sawa.


Wakati Kiongozi wa ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe akithibitisha kutoshiriki kwa chama hicho, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji aliliambia gazeti la Mwananchi kwamba kutokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokea wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 , vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) navyo havitashiriki.


Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kupitia mkutano uliovihusisha vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na Chaumma ambacho kilialikwa, havitashiriki uchaguzi huo hadi vitakapokutana na NEC na kujadiliana.


Mbowe alibainisha kuwa kutokana na kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi wa kata hizo, vyama hivyo, NEC na Serikali vilipaswa kukaa katika meza ya majadiliano, kusitisha uchaguzi wa ubunge uliopangwa kufanyika Januari 13 mwakani ili wadau wakutane kufanya tathmini ya changamoto zilizojitokeza.


Katika mkutano na waandishi wa habari jana, Zitto aliilalamikia Serikali kwa kuwakandamiza wapinzani na kutumia vyombo vyake kuwadhibiti ikiwa ni pamoja na kuwakamata viongozi wa kisiasa na kuwaweka ndani mawakala wa vyama vya upinzani.


Alisema Kamati Kuu ya chama hicho ilikaa na kutathmini mwenendo wa uchaguzi katika kata hizo na kujiridhisha kwamba CCM na Serikali ilitumia mabavu kupitia vyombo vya dola na hasa Jeshi la Polisi.


Alisema NEC ilionekana kutojali hitilafu zilizojitokeza na kuchukua hatua kurekebisha kabla ya kuitisha uchaguzi mpya.


Zitto alisisitiza kuwa, uwanja wa demokrasia umevurugwa na mchakato mzima wa uchaguzi huru na wa haki kuharibiwa.


Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja alisisitiza kuwa wameamua kususia uchaguzi huo ili kutoa ujumbe kwa wadau kuwa kuna tatizo hivyo kuwepo haja ya majadiliano.


“CCM wakifanya kama walichokifanya (kwenye uchaguzi mdogo uliopita), sisi tutafanya kama Katiba na sheria zinavyosema. Tutashiriki chaguzi zijazo, sasa tunatuma ujumbe,” alisema mwenyekiti huyo.


Katika ufafanuzi wake, Dk Mashinji alisema tangu NEC ipuuze ombi lao la kutaka kukaa katika meza ya mazungumzo, vyama vinavyounda Ukawa haviwezi kushiriki uchaguzi huo wa ubunge.


“Kwa kuwa Tume imeamua kuendelea na ratiba nyingine, vyama vinavyounda Ukawa vitaendelea na mpango wake wa kujiweka kando,” alisema.


Uchaguzi huo mdogo utafanyika katika majimbo ya Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido. Tayari CCM imeteua wagombea na CUF upande unaomuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.


Wakati huohuo, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limetoa mapendekezo kwamba ndani ya sheria na Katiba kuwepo kipengele cha kila mwanasiasa anayetaka kuhama chama ahame na cheo chake ili kuepusha gharama za kufanya uchaguzi mdogo.


Jukata ilitoa kauli hiyo kupitia tamko la kufunga mwaka lililotolewa jana na Mwenyekiti wake, Hebron Mwakagenda kwa vyombo habari kuhusu mwenendo wa matukio ya kisiasa yanayoendelea nchini, ikiwamo kuhama vyama kwa wanasiasa na uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata 43 uliofanyika Novemba 26.

Na Peter Elias na Jackline Masinde - Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527