UKATIKAJI UMEME TANZANIA MWISHO DISEMBA 15


WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema hakuna mgawo wa umeme nchini na kwamba tatizo la kukatika kwa umeme linalojitokeza maeneo mengi hivi sasa litamalizika Desemba 15, mwaka huu.

Aidha amesema tatizo hilo linatokana na kufanyika kwa marekebisho ya mitambo iliyochakaa kwa kudumu kwa takribani miaka 40 sasa.

 Akizungumza katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC 1), Dk Kalemani alisema lengo la marekebisho yanayofanywa ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mitambo itakayowezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika wakati wote.

Alisema umeme una umuhimu katika Taifa lolote likiwemo Tanzania ambalo linapambana kwenda katika uchumi wa kati wa viwanda na kusisitiza kuwa wakati wa utekelezaji wa hatua hiyo ya maendeleo ni vigumu kutenganisha na maendeleo ya nishati.

“Tuna upungufu wa umeme kutokana na ukarabati unaoendelea, mafundi hawalali kuhakikisha hali inakuwa sawa, hadi kufikia Desemba 15, mwaka huu tutakuwa tumefanya ukarabati katika sehemu kubwa na kutakuwa na tofauti kubwa,” alisema Dk Kalemani.

Aidha akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa mtambo wa uzalishaji umeme wa Kinyerezi 2 jijini Dar es Salaam, Waziri huyo alisema hadi sasa ujenzi wake umeshakamilika kwa asilimia 86 na kwamba kuanzia mwezi huu megawati 30 zitaanza kuzalishwa kila mwezi.

Alisema pia wanaendelea na mchakato wa kumpata mkandarasi atakayejenga mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge, uliopo katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,100 kwa mkupuo.

Kwa mujibu wa Waziri Kalemani matarajio ni kuwa hadi kufikia Januari au Februari mwakani, mkandarasi huyo atakuwa amepatikana na aliwataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi cha maboresho yanayoendelea.

Mbali na miradi hiyo, Dk Kalemani pia alisema mradi wa umeme wa Makambako- Songea ni moja ya miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa na utakamilika ifikapo Septemba, mwakani na utakuwa na vituo vitatu vya kupozea umeme.

Alisema hatua hiyo na nyinginezo za utekelezaji wa mpango wa usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa REA III umelenga kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2021 huku hivi sasa vijiji takribani 7,000 havijaunganishwa na huduma hiyo.

IMEANDIKWA NA OSCAR JOB - HABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527