Picha : POLISI SHINYANGA YAKAMATA WACHINA WAKIWA NA MAWE YANAYODAIWA KUWA NA MADINI


Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu sita wakiwemo raia wanne wa China kwa kosa la kusafirisha na kuhifadhi mawe yanayosadikiwa kuwa na madini kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, ACP Simon Haule watuhumiwa walikamatwa Disemba 6,2017 saa saba mchana katika kata ya Ibadakuli wilaya ya Shinyanga na askari wa usalama barabarani wakati wakikagua roli lenye namba za usajili T 209 AVH lililokuwa limebeba mawe hayo yaliyochongwa mfano wa virungu. 

Kamanda Haule alisema baada ya kuwakamata wachina hao na madereva wao, walisema mawe hayo wanayapeleka kuyahifadhi kwenye kwenye kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kula cha Jielong Tz Co . Ltd kilichopo mjini Shinyanga. 

Raia wa China waliokamatwa ni Bai Tao 40, Chen Dunlu 33, Huanran Liu na Jianhua Xiong na madereva wao wawili ambao ni Anwari Shabani na Joseph Kapoli. 

Mmiliki wa mali hizo Huanran Liu amekiri kutokuwa na lesseni wala kibali cha kusafirisha mawe hayo na kudai yeye ni mtafiti wa madini na ameyahifadhi kwenye kiwanda hicho cha mafuta kwa muda tu na hakuwa tayari kutaja wapi wameyapata.

Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati Magharibi, Hamisi Kamando amesema kuna uwezekano mkubwa wa mawe hayo kuwa na madini ya thamani ingawa hawezi kutaja ni aina gani hadi uchunguzi wa kimaabara ufanyike.

Kamando amesema kitendo cha watuhumiwa hao kukutwa na mawe hayo bila kuwa na leseni wala kibali cha kujihusisha na biashara ya madini ni kinyume cha kifungu cha 6 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa Shinyanga ACP Simon Haule akionyesha mawe waliyoyakamata yanayosadikiwa kuwa na madini ndani yake.Picha zote na Marco Maduhu – Malunde1 blog
Kamanda Haule akimhoji Jianhua Xiong ndani ya kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kupikia cha Jielong kwanini wamekiuka sheria za nchi kwa kusafirisha mawe hayo na kuyahifadhi kwenye kiwanda cha mafuta ya kula bila kibali
Trei za mawe hayo yanayosadikiwa kuwa na madini ndani yake
Trei za mawe yanayodaiwa kuwa na madini
Trei za mawe hayo 
Trei za mawe
Kamanda Haule akiwa katika gari lililokamatwa na mawe yanayosadikiwa kuwa na madini
Gari lililokamatwa na mawe yanayosadikiwa kuwa na madini lenye namba za usajili T 209 AVH mali ya Deogratius Maganga mkazi wa Tabora.
Picha zote na Marco Maduhu – Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527