MBUNGE WA UDSM ALIYEPIGA NA KUSAMBAZA PICHA ZA MAJENGO YENYE NYUFA ANYIMWA DHAMANA POLISI

 Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kumbusho Dawson anashikiliwa na polisi akituhumiwa kusambaza picha kuonyesha nyufa kwenye majengo ya hosteli.


Dawson ambaye ni mbunge wa serikali ya wanafunzi (Daruso) ameshikiliwa jana Jumatatu Desemba 4,2017 mchana.

Makamu wa Rais wa Daruso, Anastazia Anthony amethibitisha kukamatwa kwa mbunge huyo saa saba mchana.

"Ni kweli Kumbusho amekamatwa na kupelekwa kituo cha polisi cha Chuo Kikuu kwa ajili ya kuhojiwa lakini ilipofika saa tisa alasiri polisi wamesema hawana uwezo wa kumuhoji hapa hivyo watampeleka Oysterbay," amesema Anastazia.

Alipotafutwa kwa simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Murilo Jumanne hakupatikana kuzungumzia kukamatwa kwa mwanafunzi huyo.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipotafutwa amesema hana taarifa kuhusu tukio hilo.

Amesema anasubiri atakapofikishiwa taarifa atazitoa kwa umma.

Moshi Moshi, mwanafunzi wa UDSM akizungumzia kukamatwa kwa Dawson, amesema ameshughulikia dhamana yake katika Kituo cha Polisi Oysterbay lakini polisi wamesema hawezi kupewa.

Na  Fortune Francis, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post