MBUNGE WA CUF ALIYEHAMIA CCM AACHA KICHEKO NA BUMBUWAZI KWA MAALIM SEIF, LIPUMBA



Uamuzi wa Maulid Mtulia kujivua ubunge na uanachama haujakishtua chama chake cha CUF, badala yake kimesema bado wengine wawili ambao kingependa waondoke haraka.
Hilo lilisemwa jana na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anaongoza upande mmojapo kati ya mbili zinazokinzana. Upande mwingine unaongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba.
Lakini upande wa Profesa Lipumba umesema unatafakari uamuzi huo wa Mtulia ambaye anakuwa mbunge wa pili kujivua uanachama.
Wakati sakata hilo la kuhamahama vyama likipamba moto, aliyekuwa naibu waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana wa Serikali ya Awamu ya Nne, Makongoro Mahanga amesema amekuwa akifuatwa na watu tofauti ambao “pengine hawafahamiani” wakimshawishi arudi CCM, lakini amesema kamwe hataondoka Chadema.
Hamahama ya wanasiasa imesababisha baadhi ya kata kufanya uchaguzi mdogo kujaza nafasi zilizoachwa wazi na madiwani waliohamia CCM, huku jimbo moja likitarajiwa kupata mbunge mpya Januari 13 na sasa Kinondoni imekuwa wazi baada ya Mtulia kujiuzulu juzi.
Hayo yakielezwa, mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Lipumba amesema wanatafakari uamuzi wa Mtulia kujivua ubunge ghafla.
Hata hivyo, naibu katibu mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui aliliambia gazeti la Mwananchi kwa njia ya simu jana kuwa, Mtulia ni mmoja wa wabunge watatu wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.
“Hatukutarajia kama Mtulia ataondoka wakati huu, bali tulijua ataendelea kudumu. Lakini kama ameondoka ni faraja kwetu kwa sababu katika mipango yetu tulishamuondoa,” alisema Mazrui.
“Tunawaombea dua wale wawili waliobaki waondoke hata leo kwa sababu kuendelea kukaa kwao ndani ya CUF ni kukidhoofisha chama hiki.”
Mazrui aliwataka wabunge kutoshangaa endapo wenzao hao watatangaza kujiuzulu nafasi zao akidai kuna mipango inaendelea kupangwa ili kufanikisha mchakato huo.
“Narudia tena na waondoke, tena waondoke haraka. Ninawahakikishia wana CUF kuwa chama hiki kipo imara na wasiwe na hofu,” alisema Mazrui.
Alisema CUF ni taasisi imara na kati ya wabunge 40, watatu alidai wamekuwa wakikivuruga chama hicho kwa kushirikiana na Profesa Lipumba.
Akizungumzia kuondoka kwa Mtulia, alisema wakati mwingine akifa mgonjwa uliyemuuguza muda mrefu unamshukuru Mungu.
“Tunamshukuru Mungu maana tumeuguza vya kutosha. Haikuwa bahati yetu,” alisema.
Naye Profesa Lipumba alisema kamati ya utendaji ya CUF itakutana kutafakari.
“Siwezi kusema lolote kwa sasa. Bado natafakari kwa sababu nimemtafuta mhusika (Mtulia) sijampata hadi sasa. Kwa kweli imekuwa ghafla na hakuwahi kunidokezea kwamba atahama,” alisema.
“Kamati ya utendaji itakutana kujadiliana kuhusu suala hili. Naomba uwe mvumilivu tunahitaji kujua nini chanzo cha yeye kuondoka, kisha tutatoa taarifa kwa vyombo vya habari.”
Hamidu Bobali, mwenyekiti wa Jumuiya Vijana wa CUF (JuviCUF), ambayo Mtulia alikuwa naibu katibu mkuu alisema kitendo kilichofanywa na mbunge huyo kimemshushia hadhi.
Alimtaka Mtulia akumbuke namna ambavyo watu walipambana hadi akaibuka kidedea katika ubunge wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
“Tulianza kumpigania ndani ya CUF, hivi mliweza kufikiri kama Mtulia angemshinda (Abdul) Kambaya? Kambaya alikuwa na nguvu na kila sifa, lakini JuviCUF tulimpigania kijana mwenzetu ili ateuliwe kwenye kura ya maoni, ili agombee jimbo lakini matokeo ndiyo haya,” alisema Bobali ambaye pia ni mbunge wa Mchinga mkoani Lindi.
Barua ya kujiuzulu Mtulia
Katika taarifa yake ya kujiuzulu, Mtulia alitoa sababu zinazolingana na wanachama wengine waliohamia CCM, akisema chama hicho kimefanya mambo mengi ambayo wapinzani waliyaahidi.
“Kwa kuwa nia yangu ni kuwatumikia wananchi, sioni sababu ya kuendelea kuwa upinzani na badala yake nimeona ni vyema niungane na juhudi za Serikali kwa kumuunga mkono Rais Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo na kukabiliana na kero mbalimbali,” alisema.
Aliwashukuru wananchi wa Kinondoni kwa kumpa dhamana ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kuwaahidi kuwa yupo tayari kuendelea kushirikiana nao. Hadi jana, katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alikuwa hajapokea barua ya Mtulia kuhusu kujiuzulu kwake.
Dk Mahanga adai CCM inamsaka
Katika hatua nyingine, Dk Mahanga ambaye aliwahi kuwa naibu waziri kwa takriban miaka kumi, amedai kufuatwa na watu tofauti wanaomshawishi arejea CCM.
Dk Mahanga ambaye alihamia Chadema Agosti 2, 2015, baada ya kushindwa katika kura za maoni ya kuwania ubunge wa Segerea, alisema alijitoa CCM kwa sababu utaratibu uliotumika haukuwa sahihi na uligubikwa na vitendo vya rushwa na njama zilizofanywa na viongozi wa kitaifa kuhakikisha anaondolewa, lakini sasa wanamfuata.
“Siwezi kuwataja ni akina nani, wala idadi yao na mara ngapi wamekuja.  Ila umma ujue wameshakuja mara kadhaa  kunishawishi na sidhani kama wanajuana kuwa wanatumwa na kwenda kwa  mtu mmoja,” alisema Dk Mahanga.
“Nawaambia hivi sirudi huko. Huwa ninaishi kwa ninachokiamini na hakuna kinachoweza kunishawishi kubadili imani na dhamira yangu ya Agosti 2 mwaka 2015.”
Kabla ya kuzungumza na gazeti hili, Dk Mahanga aliandika katika ukurasa wake wa Facebook kuhusu harakati hizo.
“Imani yangu, utu wangu na msimamo wangu huwa hauna bei. Kamwe sitorudi CCM acheni kuhangaika,” aliandika Dk Mahanga katika ukurasa huo.
 Mwanasiasa huyo alijifananisha na kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga akisema hatabadili msimamo.
Pia alishangaa baadhi ya watu wanaotoka upinzani kwenda CCM wakidai kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli na kuunga mkono jitihada za Serikali wakati hali ya maisha ni ngumu kwa Watanzania.
Na  Bakari Kiango na Beldina Nyakeke -  Mwananchi  

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post