MBUNGE JAMES MBATIA AVUNJIKA MKONO BAADA YA KUANGUKA...ALAZWA KCMC




Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya kuvunjika mkono.


Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), amevunjika mkono wa kushoto baada ya kuteleza na kuanguka na amelazwa katika wodi za watu mashuhuri (VIP).


Msaidizi wa mbunge huyo, Hamis Hamis amesema leo Jumatano Desemba 20,2017 kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 2:45 usiku wakati akiondoka hotelini kurejea nyumbani.


Hamis amesema Mbatia alikuwa akishuka ngazi katika hoteli ya Uhuru iliyopo eneo la Shanty Town ndipo alipoteleza na kuanguka.


“Bahati nzuri pale kulikuwa na daktari wa KCMC anaiwa Ansbert Sweetbert ndiye alitoa huduma ya kwanza hadi kumpeleka KCMC,” amesema.


Amesema, “Kwa kweli huyo daktari alikuwa msaada mkubwa. Ndiye aliyempeleka KCMC na alikaa naye hadi saa nane usiku. Wauguzi na madaktari KCMC walimpa msaada mkubwa.”


Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alipotafutwa leo mchana amesema bado maumivu aliyonayo ni makali kutokana na kuvunjika mkono.


“Bado nina maumivu makali. Nashukuru sana Mungu na jopo la madaktari limeshakutana na watafanya uamuzi,” amesema.


Mbatia amesema alishapatiwa matibabu ya mwanzo baada ya vipimo vya X-Ray kuthibitisha amevunjika mkono, lakini madaktari wanafanya tathmini ni huduma gani zaidi apewe.

Na Daniel Mjema, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527