KANISA LAWAOMBEA BABU SEYA,PAPII KOCHA KWA SAA TANO





Mwanamuziki wa dansi, Nguza Viking ‘Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza, maarufu kwa jina la kisanii la Papii Kocha, wamefanyiwa maombi maalumu yaliyodumu kwa takriban saa tano baada ya kutoka gerezani kwa msamaha wa Rais.


Maombi hayo yalifanyika juzi katika Kanisa la Life in Christ Ministries Zoe, lililopo Tabata Segerea na yalianza saa 1:00 jioni hadi saa 5:00 usiku yakiongozwa na Nabii Joseph.


Nguza, ambaye ni maarufu kutokana na kibao chake cha “Seya” na Papii Kocha, ambaye walishirikiana naye kukitengeneza upya kibao hicho, walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha, lakini walitoka gerezani baada ya Rais John Magufuli kutangaza kuwasemehe wafungwa 8,157 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika zilizofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.


Wanamuziki hao walikaa gerezani kwa takriban miaka 13 na miezi minne baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi watoto 10 wa kike ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa ya Sinza jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na gazeti, Nabii Joseph alisema wamewaombea Nguza na Papii Kocha ili kuwajengea uwezo wa namna ya kuishi maisha mapya ya uraiani kama wananchi wengine baada ya kutoka kifungoni.


Alisema wakati maombi hayo yakiendelea, Nguza na Papii walionyesha kuwa wapo tayari kubadilika na kumtumikia Mungu.


“Mtu anapofungwa maisha na kuachiliwa huru, anaona kama akili inakataa kuamini kama ni kweli yupo huru. Ndio maana walivyotoka gerezani walikuja hapa ili tuwaweke vizuri,” alisema.


Nabii Joseph alitumia nafasi hiyo kueleza sababu ya Babu Seya na Papii Kocha kwenda moja kwa moja kanisani badala ya nyumbani walikokuwa wameandaliwa kwa mapumziko.


Alisema wakati wakiwa gerezani, kila wakati alikuwa akiwatumia ujumbe kupitia kwa ndugu yao Nabii Michael Nguza uliolenga kuwapa matumaini na moyo wa kuamini kuwa Mungu yupo na kwamba ipo siku watatoka gerezani kwa kuwa yeye alishaoteshwa.


“Ndiyo maana kama mnakumbuka Babu Seya aliwahi kusema kuwa akitoka gerezani ataishi maisha ya kumtumikia Mungu.Aliamua kusema hivi baada kupata ujumbe wa maono yangu kuwa Mungu anawahitaji wamtumikie,” alisema Nabii Joseph.


Nabii Joseph alidai kuwa kwa nyakati tofauti aliwahi kutabiri zaidi ya mara tatu kuwa Nguza na mwanae watatoka gerezani, hivyo anamshukuru Mungu na Rais Magufuli kwa uamuzi wa kuwachilia huru wanamuziki hao.


Kwa mujibu wa Nabii Joseph, baada ya kumaliza maombi hayo, Nguza na Papii Kocha walielekea sehemu maalumu bila kuitaja jina kwa ajili ya mapumziko ya utulivu wa Mungu.


Alisema wamepanga kuwapa ushauri wa kiroho kwa muda wa wiki moja kwa kutumia wachungaji na manabii watakaokuwa wakienda sehemu hiyo maalumu ya mapumziko,” alisema Nabii Joseph.


Mbali na hilo, Nabii Joseph alisema kanisa hilo limeandaa wimbo maalumu unaoitwa “Siku za Maisha Nilizokuwa Gereza” kwa ajili ya wawili hao.


“Wimbo huu niliutunga miaka mitatu iliyopita. Ndani ya wimbo tumshirikisha Papii Kocha sehemu ya kiitikio kinachosema “upendo wa Mungu kwa ajili ya maisha” na atatumbuiza siku ya ibada ya Jumapili ijayo akiambatana na baba yake,” alisema nabii huyo.


Alisema siku hiyo kutakuwa na ibada maalumu itakayoanza saa 3:00 asubuhi hadi jioni kwa ajili ya kumuomba Mungu na kumuombea Rais Magufuli kwa upendo wake na moyo wa huruma alionyesha kwa wafungwa 8,157 alioachia huru.


Mmoja wa waumini wa kanisa hilo, Mchungaji Petros alisema ni furaha kuwaona Nguza na Papii Kocha wakiwa huru na kuanza maisha mapya.




Ilivyokuwa baada ya kuachiwa


Baada ya Rais Magufuli kutangaza msamaha kwa wanamuziki hao, saa 11:00 jioni gazeti la hili lilizungumza na Mkuu wa Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam, (DCP), Augustine Mboje aliyesema wapo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwaachia.


Ilipotimu saa 12:00 jioni, ungeweza kusema watu waliokuwa nga’mbo ya pili ya lango kuu la gereza la Ukonga walikuwa wanashangilia mpira, bali ni shangwe za kuziona sura za Nguza na Papii Kocha wakati wakitoka.


Kiongozi huyo wa bendi ya zamani wa Marquis du Zaire na mwanae waliwapungia mikono watu waliokuwa nje ya gereza.


Ilikuwa ni furaha kwa ndugu na marafiki waliojazana nje ya gereza kila mmoja akitaka kuwaona na wengine kuwashika mkono na kusababisha msongamano wa magari.


Watu hao walisikikia wakilitaja jina la Rais Magufuli huku wengine wakimkaribisha uraiani Nguza, ambaye ni maarufu kwa upigaji gitaa la solo na mwanae ambaye ni mwimbaji.


Hali hiyo ilililamzimu Jeshi la Magereza kuingilia kati na kuwazuia watu hao kisha kuwaingiza wasanii kwenye gari na ndugu zao wa karibu.


Wakati wanatoka Nguza na mwanaye walibeba magitaa na walionekana na nyuso za furaha na msafara wao ulianza kuelekea kanisani.


Walifika kanisa hapo saa 1:00 jioni na kuamsha furaha kwa ndugu zao wa karibu ambao baadhi walikumbatiana nao.


Miongoni mwa marafiki wa karibu walioambatana na wawili hao ni mwimbaji wa kundi la FM Academia, Nyoshi El Sadat ambaye alionekana kuwa mtu mwenye furaha.


“Namshukuru sana Mungu ndiyo maana nipo hapa,” alisema Nyoshi.


“Nilikuwa nimelala nilipoamka saa 9:00 alasiri na kuangalia simu nikakuta kuna idadi kubwa ya watu walionipigia na kunitumia ujumbe mfupi. Ikanibidi nichukue gari na kwenda gerezani na tumetangu wakati huo, tupo hapa kanisani.


“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu na Rais Magufuli kwa kuwasemehe wote na si familii hii pekee. nikiongelea familia hii watasema napendelea ila tunamshukuru Rais kwa kuwaseheme wote.”


Mmoja wa watoto wa Nguza, Michael Nguza maarufu kama Nabii Michael alisema leo huenda wakatoa tamko la familia baada ya baba yake na mdogo wake kutoka gerezani.

Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post