FAMILIA YA BABU SEYA YASIMULIA UTABIRI WA NABII JOSEPH KUTIMIA KUTOKA GEREZANI
Familia ya mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ imeeleza jinsi mchungaji wa Kanisa la Life in Christ Ministries Zoe, lililopo Tabata Segerea jijini Dar es Salaam alivyotabiri kutoka gerezani kwa wanamuziki hao.


Akizungumza leo Jumapili Desemba 24 katika ibada ya kumshukuru Mungu kwa miujiza aliyoitendea familia hiyo iliyofanyika katika kanisa hilo, mtoto wa Babu Seya Michael Nguza 'Nabii Nguza’ amesema utabiri huo sasa umekuwa kweli.


Amesema mchungaji wa kanisa hilo Nabii Joseph alitabiri mara tatu kuwa ndugu zake hao wataachiwa huru.


Babu Seya na Papii Kocha wamekaa gerezani miaka 13 na miezi minne wakikabiliwa na kosa la kubaka na kulawiti watoto 10 wa kike ambao walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza Dar es Salaam.


Waliachiwa huru Desemba 9, mwaka huu kufuatia msamaha wa wafungwa, ukiwahusisha waliofungwa maisha na waliohukumiwa kunyongwa uliotolewa na Rais John Magufuli, muda mfupi baada kutoka gereza la Ukonga walikwenda katika kanisa hilo na kuombewa na Nabii Joseph kwa takribani saa tano.


Amesema nabii Joseph alitabiri kwa mara kwa kwanza mwaka 2012 na mara ya pili mwaka 2014.


“Utabiri wa tatu ulikuwa Mei 21 mwaka huu. Nabii Joseph alisema amepokea neno la Mungu lenye ujumbe kuwa watu wawili ambao ni baba na mwanaye wataachiwa huru, mmoja atakuwa kijana na mwingine mzee,” amesema na kuongeza,


"Haya mambo si ya kutunga ni ya uhalisia kwa sababu naamini Mungu yupo na nilimuamini sana Nabii Joseph kwa kile alichokuwa akitabiri na nilikuwa naipelekea familia yangu ujumbe gerezani na iliupokea.”


Na Bakari Kiango, Mwananchi
Theme images by rion819. Powered by Blogger.