DC KANALI NDAGALA AKABIDHI VIFAA VYA KISASA VYA UPALILILIAJI MPUNGA SKIMU YA KATENGERA


Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akipalilia mpunga kwa kutumia vifaa vya kisasa na wakulima wa skimu ya umwagiliaji ya mpunga - Picha na Rhoda Ezekiel Kigoma - Malunde1 blog Kigoma
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akikabidhi kifaa cha upaliliaji kwa katibu wa kikundi cha upaliliaji Yasinta Mathias
Wakulima wa Skimu ya umwagiliaji ya Mpunga ya Katengera katika kijiji cha Kinonko na Ruhwiti katika kijiji cha Nyakayenzi kata ya Kasuga wilayani Kakonko, mkoani Kigoma wametakiwa kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa zao la mpunga ili kuzalisha mazao ya kutosha kutokana na zao hilo kuwa zao kuu la biashara kwa wilaya hiyo. 

Wito huo umetolewa leo na mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala, wakati akikabidhi vifaa vya Teknolojia rahisi vya upaliliaji mpunga kwa kikundi cha upaliliaji vyenye thamani ya shilingi 12,700,000/= vilivyo tolewa na shirika LIC (Local Investment Climate).

Kanali Ndagala alisema vifaa hivyo vitatumika kupalilia katika mashamba ya mpunga katika skimu za Katengera na Ruhwiti lengo likiwa ni kuwaongezea kipato wanawake wanaojishughulisha na upaliliaji pamoja na wakulima wa mpunga kwa kuongeza uzalishaji.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaagiza wakulima hao kuongeza uzalishaji kutokana na serikali kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wakulima kwa kuwapatia msaada wa vifaa vya kilimo kama vile vifaa vya kupalilia ambapo kutokana na ukosefu wa vifaa awali walikuwa wanapata mazao machache. 

Aidha aliwataka kulima mara mbili kwa kwa mwaka na kuhakikisha kuwa ekari moja inazalisha gunia 40 hadi 45 za mpunga tofauti na kipindi ambacho walikuwa hawana nyenzo hizo.

"Niwaombe wakulima wote kulima mara mbili kwa mwaka katika Skimu hizi za umwagiliaji, Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika skimu hii, lazima mjitahidi kuzalisha ili tuweze kupata mazao ya kutosha na kuvutia wawekezaji katika viwanda vya kukoboa mpunga na kuinua uchumi wa Wanakakonko",

Kwa yeyote atakayeshindwa kulima mara mbili kwa mwaka hatutasita kuchukua shamba lake na kugawa kwa wengIne au kutafuta wawekezaji ili waweze kuwekeza zaidi na kupata mazao ya kutosha", alisema Kanali Ndagala.

Hata hivyo Kanali Ndagala aliwaagiza wakulima hao kuzingatia maelekezo ya mabwana shamba katika uwekaji wa mbolea, pamoja na kuzingatia muda wa kupalilia ili waweze kuongeza uzalishaji na kupata mazao yenye ubora zaidi.

Akikabidhi vifaa hivyo mbele ya mkuu wa wilaya kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika la RERAI linaloshughulika na kuvisaidia vikundi vya wakulima kwa ajili ya kuongeza uzalishaji katika kilimo cha mazao mbali mbali Dr. Brigton Gwamagobe, alisema waliona wakulima hao wanahangaika katika upaliliaji wa mpunga.

Alisema kufuatia changamoto hiyo waliomba wafadhili kuwasaidia kuwapa vifaa vya kupalilia ambapo wamefanikiwa kutoa vifaa 50 vyenye thamani ya milioni 12 vitakavyogawiwa katika skimu ya Katengera na Ruhwiti.

Alisema kabla ya vifaa hivyo kutolewa katika vikundi vya upaliliaji ekari moja ilikuwa ikipaliliwa kwa bei ya 135,000 kwa kila eka na sasa itakuwa ni ekari 50,000 hivyo uzalishaji utaongezeka kutokana na wakulima wengi walikuwa wanashindwa kupata mavuno ya kutosha kutokana na kutopalilia kwa wakati na kutumia kemikali kuua wadudu lakini kifaa hicho kitumika pia kuua wadudu pamoja na gharama nafuu za upaliliaji.

Kwa upande wake katibu wa kikundi cha upaliliaji Yasinta Mathias aliishukuru serikali pamoja na wawekezaji kwa kuja kuwekeza katika skimu hiyo na vifaa hivyo vitawasaidia kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na kuepukana na adha ya kuumwa na wadudu waliokuwa wakikaa kwenye maji ya mpunga pamoja na kukatwa na majani.

Alisema kwa sasa uzalishaji utaongezeka kutokana na zao hilo likipaliliwa mapema litaongeza uzalishaji kutokana na kupata nafasi ya kukua vizuri na kuepukana na majani yanayozuia zao hilo kukua kwa wakati.

Na Rhoda Ezekiel Kigoma - Malunde1 blog Kigoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post