DC AMTAKA ALIYETENGWA MIAKA 27 KWA USHIRIKINA AOMBE RADHI WANAKIJIJI


 
Mkuu wa wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amemtaka mkazi wa kijiji cha Tumati, Faustina Boay ambaye kwa miaka 27 alitengwa na wananchi wa eneo hilo kwa imani za kishirikina kuwaomba msamaha ili waishi kwa amani.


Kutokana na kutengwa na wananchi hao, Boay alipata msiba wa kufiwa na watoto wake wawili lakini alilazimika kushirikiana na mkewe kuwazika baada ya jamii ya eneo hilo kumtenga.


Akizungumza juzi kwenye mkutano na wananchi wa eneo hilo, Mofuga alimtaka Boay kuomba radhi kwa jamii ili kuendelea kuishi kindugu kama miaka iliyopita.


Alisema si jambo zuri kwa Mtanzania wa leo kujitenga peke yake na kufanya shughuli za kijamii ikiwamo kuzika watoto wake bila kusaidiwa na wananchi wanaomzunguka ikiwamo majirani zake.


“Nimemshauri aombe radhi kwa wananchi ili aishi maisha kama zamani na jamii imsamehe isimtenge tena, haya mambo ya kumuona yeye ni mpenda ushirikina yakome na kugombea mpaka wa eneo na jirani zake uishe sasa,” alisema Mofuga.


Alisema kama ni adhabu kwa mwananchi huyo imetosha na ameadhibiwa kwa muda mrefu kwa kuwa miaka 27 aliyoishi yeye na familia yake bila kushiriki shughuli za kijamii inatosha kumfanya ajirudi na kufungua ukurasa mpya wa maisha na wananchi wenzake.


Hata hivyo, Mofuga alipinga vikali kitendo cha wananchi wa kijiji hicho kuchoma nyumba ya Boay kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kulipiza kisasi wakimtuhumu kufanya ushirikina kwa kumloga jirani yake.


“Suala la kuchoma nyumba ya Boay siliungi mkono hata kidogo kwani huko ni kujichukulia sheria mkononi na ninawapongeza askari polisi waliowakamata wahusika wa tukio hilo,” alisema Mofuga.


Kwa upande wake, Boay ambaye kwa zaidi ya miaka 27 alikuwa amejitenga na jamii hiyo ikiwamo kutohudhuria sherehe au misiba inayotokea kijijini hapo, alisema ataufanyia kazi ushauri huo.


“Hata mimi nimechoshwa na maisha haya kwani jamii ilitutenga na kutuacha wenyewe mimi na familia yangu pekee, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutekeleza maagizo ya mheshimiwa mkuu wa wilaya,” alisema Boay.

Na Joseph Lyimo, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527