CCM WAELEKEZA MISHALE MAJIMBO YA UKAWA
Kuelekeza ‘mishale’ kwenye majimbo ya ubunge yanayoshikiliwa na upinzani ni moja ya majukumu waliyopewa washindi wa nafasi za juu katika uongozi wa CCM wa mikoa.


Katika chaguzi hizo, waliokuwa wasimamizi, wagombea na baadaye waliofanikiwa kushinda, wamekuwa ‘wakilishana yamini’ ya kuendesha mkakati wa kurudisha majimbo na kata walizoshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.


Lakini wakati CCM ikijipanga, Chadema imekejeli mikakati hiyo ikisema kazi hiyo itakuwa rahisi ikiwa chama hicho kitatekeleza ahadi iliyoahidi kwa wananchi ikiwamo kutoa Sh50 milioni kila kijiji na kutokujikita kueneza propaganda badala ya maendeleo.


Baadhi ya mikoa inayotolewa macho na CCM ni Mbeya, Iringa, Manyara, Arusha, Dar es Salaam ambayo upinzani ulishinda majimbo na kata nyingi iliyowafanya kuongoza halmashauri na majiji ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza uchaguzi wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995.


January Makamba aliyekuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa CCM Mkoa wa Iringa aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuchagua viongozi watakaokiwezesha chama hicho kurejesha Jimbo la Iringa Mjini linaloshikiliwa na Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema.


“Leo tunahitimisha mchakato wa uchaguzi Iringa, tunakwenda kupata safu mpya ya uongozi...uchaguzi ni fursa ya kupata safu mpya, kujipanga na kujiimarisha,” alisema waziri hiyo wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais –Muungano na Mazingira.


Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli aliongeza, “Mwaka juzi tulipata fursa ya kuondoa vichaka hapa Iringa lakini ikashindikana, katika uchaguzi huu ninaomba mchague kwa kuzingatia kuwa ipo haja ya kuwapata viongozi watakaofanikisha hilo.”


Mwenyekiti mpya aliyechaguliwa, Albert Chalamila alisema chama hicho kimepoteza mwelekeo mkoani humo kutokana na baadhi ya wanachama kuendekeza majungu, ufitini na uongo.


Alisema jukumu lililoko mbele yake sasa ni kuwaleta pamoja wanachama ili waweze kurejesha heshima ya chama hicho ndani ya Mkoa wa Iringa ambayo kwa sasa imetoweka.


“Iringa leo imepoteza majimbo matatu; Iringa Mjini, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kutokana na wingi wa kura wa Chadema wakapata mbunge wa viti maalumu… kazi iliyo mbele yetu kwa sasa ni kuhakikisha tunarejesha majimbo hayo CCM,” alisema Chalamila.


Wakati Iringa wakimaliza uchaguzi kwa ahadi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Inocent Kalogeresi baada ya kuchaguliwa tena aliahidi kuyarudisha majimbo matatu ya ubunge yaliyochukuliwa na upinzani katika uchaguzi huo wa 2015 ambayo ni Mikumi, Kilombero na jipya la Mlimba akisema yalichukuliwa kutokana na ubinafsi wa baadhi ya viongozi wa CCM na kutokuwa wamoja.


Alisema kitendo cha majimbo hayo kuchukuliwa na upinzani imekuwa ni doa kubwa katika kipindi cha uongozi wake hivyo katika awamu yake ya pili ya uongozi, atahakikisha yanarudi CCM.


“Na hata kata zilizochukuliwa na upinzani nawahakikishia zitarudi zote, naomba viongozi wenzangu tushirikiane tuache ubinafsi tutangulize masilahi ya chama,” alisema.


Mkoani Mbeya, aliyekuwa mgombea uenyekiti, Said Salmin alifichua siri ya CCM kufanya vibaya kwenye baadhi ya kata na Jimbo la Mbeya Mjini kuwa imekuwa haisikilizi na kufanyia kazi ushauri wa kitaalamu kila inapopewa.


“Mimi katika nafasi yangu nilikuwa mshauri kwa chama na nilitekeleza wajibu wangu kwa kukishauri, lakini tatizo likawa ni chama kutopokea na kupuuza ushauri na ndio sababu hakikufanikiwa.”


Baada ya kuchaguliwa, mwenyekiti mpya wa mkoa huo, Jacob Mwakasole alisema, “Natambua dhamana kubwa mliyonipa leo hii kuongoza mkoa wetu wa Mbeya, pamoja na changamoto zake. Mbeya ina changamoto za kisiasa na kijamii, lakini niseme kazi iliyopo mbele yetu sitaweza kuifanya pekee yangu, hivyo ninaomba sana ushirikiano kutoka kwenye viongozi wenzangu na wanachama wote wa Mbeya.” a


Katika hilo, mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla na mbunge wa viti maalumu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mary Mwanjelwa wamekuwa wakitaka wanaCCM kuhakikisha wanafanya jitihada kurejesha uongozi wa kichama mkoani humo.


Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 na ule wa 2015, CCM ilipoteza Jimbo la Mbeya Mjini ambalo liliangukia mikononi mwa Chadema chini ya Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Halmashauri ya Jiji la Mbeya pia iko chini ya Chadema.


Akiwa mkoani Songwe, Makalla aliwataka viongozi na wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani humo kusimama imara ili kukomboa majimbo matatu yanayoongozwa na Chadema.


Makalla ambaye alikuwa msimamisi wa uchaguzi wa umoja huo, wakati akitoa nasaha kwa viongozi waliochaguliwa, aliwataka wasione haya kukipigania chama ili kukomboa majimbo yanayoshikiliwa na upinzani kwani hilo ndilo lengo la chama cha siasa, kushika dola.


Makalla alisema UVCCM ndio nguzo ya CCM katika kuandaa viongozi wakubwa ndani ya chama na Serikali hivyo aliwataka kuwa mabalozi mkoani humo kuhakikisha majimbo ya Mbozi, Momba na Tunduma ambayo yapo chini ya Chadema yanakombolewa.


Miongoni mwa vipaumbele vya mwenyekiti aliyechaguliwa, Andrew Kadeghe ni kuwaunganisha vijana pamoja ili kubuni miradi ya kuwaletea maendeleo na kuhakikisha makundi ya uchaguzi yanafutwa lakini kubwa ni kuweka mikakati thabiti ya kukomboa majimbo ya Tunduma, Momba na Mbozi.


Mikakati hiyo ya CCM iko pia Manyara ambako Chadema inaongoza majimbo mawili ya Babati Mjini na Simanjiro kati ya saba.


Mwenyekiti mpya wa CCM wa mkoa huo, Simon Lulu akizungumza baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo mjini Babati alisema wanatarajia kurudisha heshima ya CCM mkoani humo kwa kurejesha majimbo hayo.


“Nawapongeza watu wa kata ya Nangwa Wilayani Hanang’ kwa kurudisha kata yetu iliyokuwa na diwani wa Chadema, sasa sisi wengine tujipange kuyarudisha majimbo hayo mawili,” alisema Lulu.


Imeandikwa na Ibrahim Yamola (Dar), Joseph Lyimo (Manyara), Geofrey Kahango (Mbeya) na Gefrey Nyang’oro (Iringa) - Mwananchi
Theme images by rion819. Powered by Blogger.