ASKARI MWINGINE WA JWTZ AFARIKI DUNIA KONGO


Askari wa Tanzania aliyejeruhiwa katika shambulizi lililoua wengine 14 walio katika vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ameripotiwa kufariki dunia.

Kifo hicho kinaongeza idadi na kufikia waliouawa katika shambulizi hilo kufikia 15. Askari 44 walijeruhiwa.


Umoja wa Mataifa (UN) umeelezea shambulizi hilo ni tukio baya zaidi lililovikumba vikosi vyake katika kipindi cha miaka 25.


Pia, UN imetuma rambirambi kwa Serikali ya Tanzania na ndugu waliopoteza wapendwa wao.


Katika ujumbe wa Twitter, ujumbe maalumu wa UN ulio DRC (Munusco) umesema askari huyo ni miongoni mwa waliojeruhiwa katika shambulizi la Desemba 7,2017.


Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa mbali ya kueleza kuwa, “Umoja wa Mataifa umehuzunishwa na kusikitishwa kutokana na mauaji hayo.”


Mashambulizi hayo yanadaiwa kufanywa na wapiganaji wa kundi la ADF waliojichimbia katika misitu ya Congo.


Umoja wa Mataifa umeanza uchunguzi wa kina kuhusu shambulizi hilo na umeahidi kutoa taarifa haraka iwezekanavyo.


Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix amesema uchunguzi unafanywa kwa kuzingatia vigezo vyote vya kimataifa.


Amesema baada ya kukamilika wataalamu watafanya uchambuzi na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuzuia mauaji kama hayo kujirudia.


“Uchunguzi utafanyika kwa mbinu ambazo zinatakiwa. Hitimisho na mapendekezo yatachambuliwa kwa kina na kuzingatiwa kwa hali ya juu na kwa haraka iwezekanavyo,” amesema baada ya kutembelea kambi ya Semuliki iliyoko Kivu Kaskazini.


Chanzo - Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527