TANZANIA KUONGEZA MABASI 165 YA MWENDOKASI

Tangu kuanza rasmi Mei 10, 2016 kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, zaidi ya nchi tano za Afrika zimetuma viongozi wake kujifunza namna ya uendeshaji wake.


Mfumo huo wa usafiri unalenga kupunguza foleni katika barabara, tangu uzinduliwe na Rais John Magufuli nchi za Ethiopia, Malawi, Uganda na Kenya zimetuma viongozi kuja kujifunza.


Pia, ugeni kutoka Rwanda jana uliongeza idadi ya viongozi wanaoendelea kuja mahsusi kwa ajili ya mradi huo huku kukiwa na taarifa za ujio mwingine Desemba kutoka nchini Senegal.


Akielezea utekelezaji wa mradi huo kwa wageni hao, mtendaji mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Ronald Lwakatare kuwa wanatarajia kuongeza mabasi kutoka 140 yaliyopo sasa hadi 305 katika awamu ya kwanza ya mfumo huo itakapokamilika Juni mwakani.


Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Lwakatare, inasema wageni hao sita kutoka Serikali ya Rwanda wana ziara ya siku tano kujifunza namna wakala huo unavyotoa huduma.


Lwakatare alisema ongezeko la mabasi kutasaidia kuongeza idadi ya abiria kutoka 200,000 wanaohudumiwa sasa kwa siku hadi kati ya 400,000 na 500,000. 


“Licha ya hilo, tutaongeza njia za mlisho kutoka mbili zilizopo sasa hadi tisa zitakazokuwa zikienda Masaki, Sinza, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na maeneo mengine ambayo yapo jirani ili kupanua huduma ya usafiri kwa maeneo yaliyomo ndani ya mfumo wa mabasi yaendayo haraka katika awamu ya kwanza ya mradi,” alisema.


Kuhusu athari zilizotokana na mvua iliyonyesha Oktoba 26, Lwakatare alisema mabasi 20 yaliharibika zaidi lakini yameshatengezwa na yanatoa huduma.


Alisema Dart imejipanga kuhakikisha mitaro yote inayozunguka karakana ya Jangwani inasafishwa, ili kuepuka eneo hilo kukumbwa tena na mafuriko.


Naye kiongozi wa ujumbe huo kutoka Mamlaka ya Halmashauri ya Jiji la Kigali, Rwagatore Etienne alisema wamechagua kutembelea wakala huo kwa sababu ndiyo mradi uliofanikiwa barani Afrika na upo karibu na Rwanda.


Katika msafara huo, Etienne ameambatana na wataalamu washauri ambao waliopewa kazi ya usanifu wa Jiji la Kigali ili liweze kuwa na mfumo wa mabasi yaendayo haraka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527