Picha : WAANDISHI WA HABARI WATEMBELEA VITUO VYA UTAYARI WA KUJIUNGA DARASA LA KWANZA SHINYANGA


Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Novemba 10,2017 wametembelea vituo vya utayari wa kujiunga darasa la kwanza katika manispaa ya Shinyanga ili kujionea hali ya mazingira katika vituo hivyo. 

Vituo vilivyotembelewa na waandishi wa habari ni kituo cha Ilubalo kilichopo katika kijiji cha Ilubalo kata ya Ibadakuli,kituo cha Mwagala katika kijiji cha Bushola kata ya Mwamalili pamoja na shule ya msingi Ng’wihando yenye wanafunzi waliotoka katika vituo vya utayari. 

Vituo hivyo kwa mujibu wa Mkufunzi wa walimu wa madarasa ya utayari wilaya ya Shinyanga Gideon Stephano ni miongoni mwa vituo 44 wilayani humo vilivyoanzishwa na Mpango wa kuinua ubora wa elimu nchini (EQUIP – Tanzania). 

Waandishi hao wa habari wamejionea mbinu za ufundishaji unaotumiwa na walimu jamii katika kuwafanya watoto wapende shule ambazo ni kutumia njia ya kuimba,kufundisha hadithi na kuonesha michoro mbalimbali. 

Mwalimu Lucy Cosmas wa kituo cha Ilubalo na Martine Julius wa kituo cha Mwagala walisema ufundishaji wao siyo wa kuwafundisha watoto kujua kusoma na kuandika bali wanafundisha hadithi na nyimbo mbalimbali. 

“Tunapokea watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 7 ambao huwa tunawafundisha kwa muda wa miezi mitatu kwa ajili ya kuwaandaa kuanza masomo ya darasa la kwanza”,walieleza. 

Walisema vituo hivyo vimeanzishwa kutokana na shule kwenye maeneo hayo kuwa mbali hivyo kupitia vituo hivyo watoto wanapewa hamasa ya kupenda shule. 

Hata hivyo walizitaja changamoto katika vituo hivyo kuwa ni ukosefu wa majengo ya kudumu,matandiko (sehemu za kukalia wanafunzi),vyoo na mishahara kwa walimu ambao hufanya kazi kwa kujitolea. 

Kaimu Afisa elimu mkoa wa Shinyanga Mariam Ally alisema vituo vya utayari vinasaidia kwa kiasi kikubwa kuwaandaa watoto kujiunga na masomo ya darasa la kwanza. 

“Tunaomba wazazi wawalete watoto katika vituo hivi vilivyopo karibu na maeneo yao ili waweze kujifunza,hizi changamoto zilizopo tutaendelea kuzishughulikia ikiwemo kuishawishi serikali itenge bajeti kwa ajili ya vituo vya utayari”,aliongeza Ally. 

Naye Kiongozi wa Mpango wa kuinua ubora wa elimu nchini (EQUIP – Tanzania),mkoa wa Shinyanga Archad Ruyange alisema vituo vya utayari vilianzishwa mwaka 2015 ambapo mpaka sasa kuna vituo 335 katika mkoa wa Shinyanga. 

“Tangu kuanzishwa kwa mpango huu wa vituo vya utayari tumefanikiwa kusajili watoto zaidi ya elfu 10,wazazi wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuleta watoto katika vituo hivi”,alisema Ruyange. 

Tumekuwekea picha za matukio yaliyojiri wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika vituo vya utayari vilivyopo katika manispaa ya Shinyanga
Muonekano wa jengo la kituo cha utayari cha  Ilubalo katika kata ya Ibadakuli katika manispaa ya Shinyanga.Kituo hiki kilianzishwa mwaka 2015 kikiwa na watoto 85,mwaka 2016 kilikuwa na watoto 63 na mwaka huu kina watoto 39 ambao wanaandaliwa kuingia darasa la kwanza mwaka ujao
Mwalimu Lucy Cosmas wa kituo cha Ilubalo akicheza na watoto darasani
Mwalimu Lucy Cosmas akiwasimulia hadithi wanafunzi wake
Waandishi wa habari wakiwa ndani ya darasa la mwalimu Lucy Cosmas
Mwalimu akiendelea na somo
Vitabu vya hadithi vinavyotumika kufundishia watoto 
Michoro mbalimbali katika kituo cha utayari cha Ilubalo
Mwalimu Lucy Cosmas akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kituo cha utayari cha Ilubalo
Mwalimu Lucy Cosmas akicheza na wanafunzi wake nje ya darasa
Jengo la kituo cha Mwagala katika kijiji cha Bushola kata ya Mwamalili
Mwalimu Martine Julius akiwa na wanafunzi wake katika kituo cha utayari cha Mwagala katika kata ya Mwamalili
Mwalimu Martine Julius akifundisha watoto kuimba
Mwalimu Martine Julius akieleza changamoto zilizopo katika kituo hicho ambazo ni pamoja na paa la jengo kutoboka hali inayosababisha maji kujaa darasani wakati wa mvua lakini pia kituo hicho hakina choo
Wanafunzi wakimsikiliza mwalimu Martine Julius
Waandishi wa habari wakiwa katika darasa hilo
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bushola,Sebastian Pius Salamba akiongea na wanafunzi wa kituo cha utayari cha Mwagala.Shule ya msingi Bushola ndiyo inalea kituo cha utayari cha Mwagala
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bushola,Sebastian Pius Salamba akizungumza na mwandishi wa habari wa Radio Faraja na DW,Veronica Natalis ambapo alisema  vituo vya utayari vinasaidia watoto kujifunza na kuwa tayari kujiunga na darasa la kwanza
Mmoja wa wazazi wa watoto wanasoma katika kituo cha utayari cha Mwagala bi Maria Katambi akiwaeleza waandishi wa habari jinsi kituo hicho kinavyosaidia kutoa elimu kwa watoto
Hili ni moja ya madarasa katika shule ya Msingi Ng'wihando iliyopo Old Shinyanga ambayo ni miongoni mwa shule zinazopokea watoto wanaotoka katika vituo mbalimbali vya utayari katika manispaa ya Shinyanga
Wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Ng'wihando wakiwa darasani ambapo waliosimama wametoka katika vituo vya utayari
Mwalimu Mariam Misai akieleza changamoto wanazopata wanafunzi waliotoka katika vituo vya utayari kuwa ni kusafiri umbali mrefu kwenda shuleni na kuomba serikali kujenga shule katika maeneo ambayo kuna vituo vya utayari
Kiongozi wa Mpango wa kuinua ubora wa elimu nchini (EQUIP – Tanzania),mkoa wa Shinyanga Archad Ruyange akielezea kuhusu faida za kuwa na vituo vya utayari
Kiongozi wa Mpango wa kuinua ubora wa elimu nchini (EQUIP – Tanzania),mkoa wa Shinyanga Archad Ruyange akizungumza na waandishi wa habari
Kaimu Afisa elimu mkoa wa Shinyanga Mariam Ally akizungumza na waandishi wa habari 
Mkufunzi wa walimu wa madarasa ya utayari wilaya ya Shinyanga Gideon Stephano akizungumza na waandishi wa habari.

Picha zote na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Theme images by rion819. Powered by Blogger.