Picha : SAVE THE CHILDREN YATOA MAFUNZO YA UCHUNGUZI WA KISAYANSI MATUKIO YA UKATILI WA KIJINSIA SHINYANGA


Shirika la kimataifa la Save The Children limetoa mafunzo ya ukusanyaji wa vielelezo kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi kwa ushahidi mahakamani kwa watoa huduma idara ya afya,maafisa ustawi wa jamii, waendesha mashtaka na askari polisi wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa Shinyanga.

Lengo la mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa siku tano ambayo yamefanyika katika ukumbi wa Empire Hotel mjini Shinyanga ni kuwajengea uwezo watoa huduma wa afya,ustawi wa jamii,sheria na polisi juu ya namna bora ya kuwezesha kutoa huduma kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Washiriki wa mafunzo hayo wametoka katika halmashauri ya Mji wa Kahama,Manispaa ya Shinyanga na Shinyanga Vijijini.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo leo Ijumaa Novemba 10,2017 ,Mratibu wa Ulinzi wa mtoto,haki za watoto na utawala kutoka Shirika la Save The Children Alex Enock ,alisema watuhumiwa wa kesi nyingi za ubakaji wamekuwa wakiachiwa huru kutokana na sababu ya kukosekana kwa ushahidi na hivyo kusababisha matukio hayo kuendelea kutokea.

“Baada ya kubaini sababu hizi za kukosekana kwa ushahidi usioacha shaka kwenye kesi za ubakaji ,ndiyo tumeamua kutoa mafunzo haya ya kuwawezesha wahusika wakuu ambao hushughulika na kesi hizo namna ya kukusanya vielelezo vya ushahidi na kuvipeleka mahakamani ambavyo vitamtia hatiani mtuhumiwa,ili kukomesha vitendo vya kikatili katika jamii”,alieleza Enock.

Alisema mafunzo hayo yanahusu ukusanyaji wa vielelezo kwa ajili uchunguzi wa kisayansi kwa ushahidi wa mahakama ( forensic evidence), jinsi ya kumshughulikia ikiwa pamoja na kumfanyia vipimo kwa ajili ya tiba (medical examination), utoaji wa ushahidi mahakaman, ujazaji wa fomu, pamoja na ukaguzi na ukusanyaji wa vielelezo katika eneo la tukio la uhalifu ( crime scene management)na hatimaye kupatikana kwa ushahidi usioacha shaka.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni mtaalamu wa maabara kutoka kituo cha afya cha Nindo Shinyanga Vijijini Michael Lushinge, alisema mafunzo hayo yamemuongezea utaalamu wa kuzalisha sampuli za ushahidi wa kesi za ubakaji kwa njia hizo za kisayansi ambazo zitaisaidia mahakama kuendesha kesi hizo za ukatili.

Alisema moja ya changamoto ambayo amekuwa akikumbana na nayo kwenye utendaji kazi wa kesi hizo za ubakaji ni muathirika kuwa na uelewa mdogo namna ya kuhakikisha anatunza ushahidi wake ambapo wengi wao wamekuwa wakioga na kusababisha ushahidi kukosekana.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo,mgeni rasmi SSP Lutusyo Mwakyusa aliyemwakilisha kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule, aliwataka washiriki hao kwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo hayo ili kuhakikisha watuhumiwa wa ukatili huo wa kijinsia wanafungwa jela.

Alisema bado mkoa wa Shinyanga unakabiliwa na matukio hayo ya ukatili wa kijinsia hivyo kupitia mafunzo hayo,matukio hayo yatapungua kama siyo kumalizika kabisa.

Mwakyusa aliyataka mashirika na taasisi mbalimbali zinahusika na masuala ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia waungane na wafanye kazi kwa ushirikiano ili kutokomeza vitendo hivyo.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mratibu wa Ulinzi wa mtoto,haki za watoto na utawala kutoka Shirika la Save The Children Alex Enock akielezea lengo mafunzo ya ukusanyaji wa vielelezo kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi kwa ushahidi mahakamani kwa watoa huduma idara ya afya,maafisa ustawi wa jamii, waendesha mashtaka na askari polisi wa dawati la jinsia yaliyofanyika katika ukumbi wa Empire Hotel Mjini Shinyanga kuanzia Novemba 6 hadi 10,2017 - Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Mratibu wa Ulinzi wa mtoto,haki za watoto na utawala kutoka Shirika la Save The Children Alex Enock akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.Kulia ni mgeni rasmi SSP Lutusyo Mwakyusa aliyemwakilisha kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule.
Mgeni rasmi ,SSP Lutusyo Mwakyusa aliyemwakilisha kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo
Washiriki wa mafunzo hayo wakisikiliza nasaha za mgeni rasmi
Mgeni rasmi ,SSP Lutusyo Mwakyusa akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo
Mgeni rasmi ,SSP Lutusyo Mwakyusa akimtambulisha mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto la jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Mary Sungi kwa wadau walioshiriki mafunzo hayo
Meneja wa Shirika la Save The Children Mkoa wa Shinyanga Benety Malima akizungumza wakati mafunzo ya ukusanyaji wa vielelezo kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi kwa ushahidi mahakamani  ambapo aliahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kutokomeza ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga
Meneja wa Shirika la Save The Children Mkoa wa Shinyanga Benety Malima akiwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuyatumia vyema ili kuisaidia jamii
Mwenyekiti wakati wa mafunzo hayo,Joseph Christopher kutoka dawati la jinsia na watoto mkoa wa Shinyanga akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo
Afisa ustawi wa jamii manispaa ya Shinyanga, Mary Okama akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo ambapo alisema ili kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kinachotakiwa ni ushirikiano miongoni mwa polisi,madaktari,viongozi wa serikali za mitaa,wanasheria na watu waliofanyiwa vitendo vya ukatili
Mwendesha mashtaka wa jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga Issa Ramadhani ambaye ni mkaguzi msaidizi wa jeshi la polisi akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo ambapo alisema mafunzo hayo yamemsaidia namna ya kuendesha kesi kwa kushirikiana na madaktari na wadau wengine
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini kilichokuwa kinaendelea ukumbini
Wadau wakiwa ukumbini
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini
Afisa ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Elizabeth Mweyo akiandika dondoo muhimu wakati wa mafunzo hayo
Maafisa kutoka dawati la jinsia na watoto la jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea wakati wa mafunzo hayo
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini
Picha ya pamoja baada ya mafunzo kufungwa.
Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog
Theme images by rion819. Powered by Blogger.