ATUPWA JELA MIAKA MITATU KWA KUTAPELI WATU AJIRA ZAIDI YA 140 NA KUJIPATIA FEDHA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Katavi imemhukumu Kapeele Mpundililwa (36)   Mkazi wa Namanyere wilayani Nkasi kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha kiasi cha zaidi ya Tshs  3,980,000 kwa njia ya kuwadanganya watu 144 ajira kwenye taasisi ya APAPO.

Hukumu hiyo ilitolewa hapo juzi  na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Katavi Odira Amworo baada ya Mahakama kuridhika pasipo shaka yoyote na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Awali katika kesi hiyo mwendesha mashtaka   mwanasheria wa serikali wa mkoa wa Katavi Peter Maiko alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo hapo Mei 23 mwaka huu wilayani Mpanda kwa nyakati tofauti.

Mwanassheria huyo alidai kuwa mshitakiwa Kapeele alifika Wilayani Mpanda na kujitambulisha kuwa yeye ni Mkurugenzi ya taasisi ya Shirika la Umoja wa Watu wa Afrika APAPO na alianza kutangaza nafasi mbalimbali za ajira kwa ajiri ya kampuni hiyo.

Miongoni mwa njia alizotumia kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu aliwataka kila mwombaji anaye taka kuajiriwa na taasisi hiyo ilikuwa ni lazima alipie ada ya kuombea ajira ambazo alikuwa amezitanga.

Mwanasheria Peter Maiko alieleza Mahakama kuwa kwa ngazi ya Mtaa na Wilaya kiwango cha ada ya maombi ya ajira ilikuwa ni Tshs 17,000 na sifa ilikuwa ni mtu awe na elimu ya darasa la saba hadi kidato cha nne na ajira ya ngazi ya mkoa ada ilikuwa ni Tshs 160,000 na anaeomba ajira awe na sifa ya stashahada.

Alidai kuwa mshitakiwa huyo katika utapeli huo alifanikiwa kuwadanganya watu 144 ambao waliolipia ada za maombi ya ajira hizo na kujipatia kiasi cha Tshs 3,980,000 ambazo zote ziliingizwa kwenye akaunti aliyokuwa amewapatia na shughuli hiyo ya kutafuta watu kwa ajiri ya ajira alikuwa akifanya yeye pamoja na wasaidizi wake wanne ambao walitoroka baada ya mkurugenzi wao Kapeele kukamatiwa huko Mkoani Kigoma baada ya kuwa ametoroka Mpanda.

Akisoma hukumu hiyo hakimu Mkazi Odira Mworo aliieleza Mahakama kuwa kutokana na mwenendo mzima wa kesi hiyo na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo na upande wa mashitaka mahakama pasipo shaka yoyote ile imemtia mshitakiwa hatiani .

Hakimu Amwolo alieleza kuwa miongoni mwa ushahidi uliomtia hatiani mshitakiwa ni hati za waliotapeliwa ajira walizolipia banki ambazo zililetwa Mahakamani hapo huku zikiwa na majina ya waliotapeliwa ajira na kiasi cha fedha walizoingiza kwenye akaunti ya mshitakiwa

Alisema mshitakiwa amepatikana na hatia ya kifungu cha sheria namba 302 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 ya marekebisho ya mwaka 2002 hivyo Mahaka imemuhukumu mshitakiwa Kapeele Mpundililwa kutumikia jela kifungo cha miaka mitatu jela kuanzia jana.

Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog Katavi
Theme images by rion819. Powered by Blogger.