NYUMBA YA MAJANI 'NGONDANO' YAUNGUA NA KUUA WATOTO WAWILI KAKONKO MKOANI KIGOMA


Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akikagua nyumba za majani za Ngondano zilizosababisha vifo vya watoto katika kijiji cha Luhuru wilayani humo-Picha na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia katika Kijiji cha Luhuru Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma baada ya nyumba ya nyasi/majani  'maarufu Ngondano' waliyokuwa wanaishi kuungua moto.

Kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji hicho,Bahati Kimpaye alisema tukio hilo limetokea Novemba 12 mwaka huu majira ya saa tano asubuhi baada ya nyumba hiyo kuungua na kusababisha vifo vya watoto wawili ambao ni Elizabeth Masumbuko (4) na Subira Masumbuko (2).

Alisema watoto walikuwa wameachwa ndani ya nyumba hiyo peke yao ambapo mama yao alikuwa ameenda kuchota maji.

Kimpaye alisema alipofika eneo la tukio alikuta mabaki ya neti na miili ya watoto hao ikiwa imeungua vibaya.

Alisema  chanzo cha ajali hiyo ni moto ulioshika katika nyumba ya nyasi waliyokuwemo watoto hao na watoto hao baada ya kuona moto waliingia ndani ya neti kujificha na kupelekea vifo hivyo.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala aliwaagiza wananchi wote kujenga nyumba bora za kuishi na kuacha tabia ya kuishi kwenye nyumba zilizo jengewa na majani zinazohatarisha usalama wao.

"Inasikitisha sana na ni jambo la aibu watu wana nguvu za kuchukua udongo na kujenga nyumba nzuri za kuishi lakini wengi wa wanakijiji wanaishi katika nyumba za majani hali inayohatarisha maisha yenu na kuwapoteza watoto maisha na kushindwa kutimiza ndoto zao",alisema.

"Nitoe agizo kuanzia leo sitaki kuona nyumba za majani katika wilaya hii kuliko kuishi kwenye nyumba hizi ni bora mkakaa nje ijulikane tu hamna nyumba, kuliko nyumba hizi, inaumiza sana kupoteza watoto wetu kutokana na uzembe wa baadhi ya mna nguvu za kujenga , kama mmeshindwa basi muweke utaratibu wa kujengeana kwa awamu ili kijiji chote kiwe na nyumba zenye ubora", alisema Kanali Ndagala.

Aidha Mkuu huyo aliwaomba wananchi kuacha kuwakaribisha wahamiaji haramu ambao wengi wao hujenga nyumba za majani ili watakapofukuzwa wasipate hasara na wengi wao wanasababisha matatizo makubwa katika vijiji wanavyofikia na kuwataka watoe taarifa dhidi ya wakimbizi wote.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 Kigoma
Theme images by rion819. Powered by Blogger.